Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa takribani 166 kutoka kwenye Kata 34 za Halmashauri ya Wilaya Masasi wamepatiwa mafunzo yenye Lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu Yao wanapowatumikia Wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa Leo tarehe 16/12/2024 na Wakufunzi Kutoka Chuo Cha Serikali za Mitaa Cha jijini Dodoma, ambapo pamoja na kuwajumuisha wenyeviti wa vijiji/ Mitaa pia Watendaji wa Vijiji na Kata ambao ndio wasimamizi wakuu wa Shughuli za Maendeleo nao wameshiriki kwenye mafunzo hayo yaliyofanyikia katika viunga vya Shule ya Sekondari ya wasichana Masasi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Masasi mhe.Lauter Kanoni ambaye ndiye mgeni rasmi Katika Shughuli hiyo amesema kwamba " Kwanza Kabisa nawapongeza wenyeviti wote wapya kwa kuchaguliwa na hivyo nakipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM ) kuwa katika Vijiji vyote 166 vya Halmashauri ya Wilaya Masasi kwenye Uchaguzi Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka kidedea, hongereni sana...."
Ameongeza kuwa kwasasa wenyeviti hao tayari wamekula kiapo na kiapo Chao kikubwa ni kuwatumikia Wananchi wote bila kujali dinj, kabila wala Vyama vyao hivyo hatarajii kuona wanafanya hivyo na endapo watabainika basi watakuwa wamekosa sifa ya kuwa kiongozi Bora.
Aidha suala la utunzaji wa siri nalo limesisitizwa hapa ambapo mhe.Mkuu wa Wilaya amesema ukishakuwa kiongozi lazima utunze Siri, inawezekana Wananchi mbalimbali wakaleta malalamiko Yao, na mengine inawezekana yanahusu masuala ya ndoa hivyo Kama mwenyekiti hupaswi Kutoa Siri hadharani na Kwa kufanya hivyo itakuwa ni sehemu ya kukosa maadili ya Uongozi na serikali ikikubaini ni Kweli unatoa Siri za Serikali hapo utakuwa umekosa sifa za kuwa kiongozi, na kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa Mkuu wa Wilaya nina mamlaka ya kumuondoa mwenyekiti , hakikisheni mnatunza Siri"..... alisisitiza mhe.Kanoni
Pia mhe.Kanoni akatumia fursa hiyo pia kuwakumbusha wenyeviti hao kuwa na desturi ya kuwasomea Wananchi taarifa ya Mapato na matumizi Kila baada ya miezi 3 kwani kutofanya hivyo ni moja ya sifa inayoweza ikakuondoa kwenye uongozi.
Amesema Katika Halmashauri ya Wilaya Masasi tatizo kubwa ambalo limeshamiri ni viongozi kutosoma taarifa za mapato na matumizi hivyo naagiza kuanzia sasa utaratibu huo ufuatwe Naye pia atafuatilia.
Nao kwa upande wao baadhi ya wenyeviti hao wamewashukuru wawezeshaji kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo kwa namna moja ama nyingine yamewapa mwanga mkubwa Kujua majukumu Yao ni yepi, kufahamu mipaka ya kazi zao n.k.
Jumla ya mada 09 zimewezesha kwa washiriki hao huku zikiwemo suala la Sheria za uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Miundo, majukumu na Madaraka ya vijiji, Mitaa,na Vitongoji, Uongozi na utawala bora , Uendeshaji wa vikao na mikutano katika ngazi za Vijiji, mitaa na vitongoji,Uibuaji, upangaji na usimamizi wa miradi Shirikishi ya kijamii, Usimamizi na udhibiti wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Usimamizi wa ununuzi, Usimamizi wa Ardhi na udhibiti wa uendelezaji miji na mada ya tisa ni masuala mtambuka.
16/12/2024
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa