Wenyeviti wa vijiji Halmashauri ya Wilaya Masasi wametakiwa kuhakikisha wanafanya mikutano mara kwa mara ya Wananchi na kuwasomea utekelezaji wa Shughuli mbalimbali zilizofanyika tangu walipoingia madarakani mpaka Sasa.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Masasi mhe.Lauteri John Kanoni katika kikao cha baraza la Madiwani liliofanyika hivi karibuni Wilayani humo ambapo amesema maelekezo kutoka ngazi za juu tayari yametolewa yakimtaka kila Mwenyekiti wa Kijiji aitishe mkutano wake na asome utekelezaji huku akielezea mafanikio ya CCM, kwamba tangu ilipoingia madarakani mpaka Sasa kwenye kijiji chake yamefanyika mambo gani na changamoto zilizobakia zinatatuliwa kwa namna gani ili wananchi wajue.
Amesema kwa taarifa alizonazo wenyeviti wengi hawafanyi mikutano na hawasikilizi kabisa kero za Wananchi hali ambayo inawapa ugumu wananchi kutotambua Serikali yao imewafanyia Maendeleo gani.
Ameongeza kuwa ili kulisimamia hilo ifikapo mwishoni mwa mwezi wa nane/ 2024, Wilaya itafungua jalada la Halmashauri ya Wilaya na vijiji vyote 166 vinatakiwa vitoe muhtasari wa vikao vya wenyeviti wa Vijiji ambao ndani yake utaeleza Shughuli alizozifanya tangu alipoingia madarakani mwaka 2019 mpaka juni 2024 .
Aidha mhe.kanoni amehitimisha kwa kuendelea kuwaomba waheshimiwa Madiwani nao wasibweteke kwa kumsubiria mkuu wa Wilaya kupita katika maeneo yao na kusikiliza kero za Wananchi kwani wao pia ni viongozi kwaiyo wakaanze kusikiliza na kutatua kero za Wananchi kwani zingine zipo kwenye uwezo wao wazitatue.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ndg.Ibrahim Chiputula amewasisitiza waheshimiwa Madiwani kulipa kipaumbele suala la kusikiliza kero za Wananchi "tukafanye mikutano kwenye maeneo yetu, unaweza ukakuta Mtendaji wa Kata na Diwani hawajawahi kufika kwenye Vijiji na huu mwaka wa nne, kwaiyo tukafanye mikutano na kusikiliza shida za Wananchi" alisisitiza Mhe.Chiputula.
Na: Winifrida Ndunguru
...Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa