Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt.Stergomena L.Tax katika muendelezo wa ziara yake ya siku tano katika Mkoa wa Mtwara ya kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya Maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara leo tarehe 09/10/2024 ameweka jiwe la msingi katika jengo la Wagonjwa wa nje OPD katika Zahanati ya Maparawe, Kata ya Mchauru Halmashauri ya Wilaya Masasi.
Akizungumza na Wananchi ambao wamejitokeza kushuhudia tukio hilo, Waziri Tax amewashukuru na kuwapongeza wakazi wa Maparawe kwa kushiriki kikamilifu katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huo wa zahanati ambao unakwenda sasa kuwanufaisha wakazi zaidi ya elfu nne (4000)
ambao kabla ya mradi huo wakazi wa Kijiji hicho walikuwa wakitembea umbali mrefu takribani kilomita 10 hivi kufuata huduma hiyo katika vijiji jirani.
Amesema "nipo hapa kumwakilisha mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujionea jinsi mnavyoendelea pia kuona kero za Wananchi zinatatuliwa na mahitaji yote ya kuwaletea maendeleo Wananchi yanafanyika, basi mimi binafsi nimefarijika kuona mlivyotoa michango yenu, hivyo nawashukuru sana na kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya si katika zahanati hii tu bali katika miradi mbalimbali ya maendeleo, nimetembea kote nilikozindua miradi lakini huu ndio mradi wa mfano kwasababu mmeweka nguvu kubwa sana, hongereni sana na hivi ndivyo inavyotakiwa twende na katika miradi mingine"...alisema Waziri Tax
Aidha, Mheshimiwa Tax ameongeza kuwa "mmeweka nguvu ya takribani milioni 11 na Serikali baada ya kuona dhamira yenu ya dhati mheshimiwa Rais akaelekeza kiasi cha shilingi Milioni 50 zifike hapa, kwaiyo hapa mmechangia takribani asilimia 15 hadi 20, kwaiyo niwapongeze sana".
Hata hivyo pamoja na pongezi hizo, mheshimiwa Waziri ametumia fursa hiyo kuwaomba Wananchi wa Maparawe kuitumia vizuri zahanati hiyo (waitunze) huku naye akihaidi kuwachangia shilingi Milioni 2 ili waendelee na ujenzi wa eneo la kukaa Wagonjwa wanaposubiria kupatiwa huduma.
Ifahamike kuwa kabla ya mradi huo wa zahanati wakazi wa kijiji hicho walikuwa wakitembea umbali mrefu wa takribani kilometa 10 kwenda vijiji jirani kufata huduma hiyo ya Afya, Bi.Suzan Khatib ni miongoni mwa wakazi wa maparawe ameishukuru serikali kwa kuwajengea Zahanati hiyo ambayo itakuwa msaada mkubwa kwa jamii nzima hususani wanawake kwani kabla ya kukamilika kwa zahanati hiyo walilazimika kufuata huduma za afya kwenye vijiji vya jirani.
Aidha zahanati hiyo inatoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za Wagonjwa wa nje, Vipimo vya maabara, huduma ya kujifungua, huduma za Watoto, upasuaji mdogo,huduma za sindano na huduma za uzazi wa mpango.
Katika hatua nyingine waziri huyo, amezulu kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa katika kata ya Lupaso Halmashauri ya Wilaya Masasi.
09/10/2024
@.. Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa