Katika kuboresha utoaji wa elimu bora katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi wadau wote wa elimu ikiwemo Wazazi, Viongozi wa ngazi zote, Jamii na mashirika kwa ujumla lazima kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha mazingira ya kujifunza na kujifunzia yanakuwa bora ikiwemo kujenga miundombinu na utoaji wa chakula shuleni hasa kwa shule za kutwa ili kuwawezesha wanafunzi kusoma vizuri.
Mkuu wa Wilaya wa Masasi Mhe Selemani Mzee (aliyesimama) akiongea na wadau wa elimu baada ya kupokea ripoti ya ufuatiliaji wa rasilimali fedha za umma kwa shule 20 za Masasi iliyowasilishwa na shirika la Haki Elimu kupitia mtandao wa Marafiki Elimu wa masasi (MEMA) katika ukumbi wa halmashauri
Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Masasi mhe. Selemani Mzee baada ya kupokea taarifa ya ufuatiliaji wa fedha za umma kwa shule 20 za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi iliyotolewa na shirika la Haki Elimu kupitia Mtandao wa Marafiki wa Elimu Masasi (MEMA) ambayo pamoja na mambo mengi imebainisha kuwa moja ya changamoto inayozikumba shule za msingi na sekondari ni upungufu na uchakavu wa miundombinu ikiwemo madarasa na ameeleza kuwa, ujenzi wa miundombinu ya shule unahusisha wadau wote wa elimu yaani serikali na jamii kwa ujumla
“Kila mmoja aone kuwa suala la wanafunzi kusomea nje au kwenye miti halikubaliki, hivyo shule ambazo zinachangamoto ya wanafunzi kusomea nje zitatafutiwa ufumbuzi wa haraka wakati ujenzi wa madarasa unaendelea” alisema Mkuu wa Wilaya.
Wadau wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) baada ya kupokea ripoti
Kuhusu matumizi sahihi ya fedha za ruzuku ambazo zina kipengere cha ukarabati wa miundombinu Selemani amewakumbusha walimu kufanya matumizi kwa kuzingatia miongozo ili fedha hizo ziweze kutekeleza shughuli zilizopo kwenye mpango ikiwemo kukarabati miundombinu na shughuli zingine za elimu na si vinginevyo.
Pia Mkuu wa Wilaya amefafanua kuwa, Wazazi wataendelea kushirikishwa kuchangia kwa hiari katika maeneo ambayo fedha ya ruzuku hazigusi ikiwemo utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za kutwa, mavazi, na mambo mengine ambayo wazazi kupitia kamati za shule itaona inafaa kwa malengo ya kuboresha elimu katika shule zao.
Mdau wa elimu akitoa mchango wake
Akitoa maelezo ya awali katika kikao hicho Mratibu wa Programu ya Haki Elimu Joyce Mkina alieleza kuwa ripoti hiyo inalenga kuwaeleza wadau wa elimu Masasi changamoto zilizopo kwenye shule ili kuona namna ya kuzitatua na hatimaye utoaji wa elimu kuwa bora jambo ambalo ndilo lengo kuu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mhe. Juma Satmah amewaeleza wadau wa elimu wakiwemo Wazazi, Walimu, Wajumbe wa bodi na kamati za shule, Watendaji wa Kata na Vijiji kuwa kwa muda mrefu hali ya miundombinu ya shule imekuwa si mizuri kutokana na mfuko wa elimu kusitishwa lakini kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imeweza kukusanya na kupeleka milioni 494 kwenye shule kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule kupitia mfuko wa elimu, hivyo baada ya muda tatizo la upungufu miundombinu na ile michakavu katika shule litakwisha kabisa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mhe. Juma Satmah akichangia jambo kwenye kikao cha wadau wa elimu
Satmah amewashukuru shirika la twaweza kwa ripoti yao ya utafiti katika shule 20 kwani imetusaidia kuona mapungufu yaliyopo na kuweza kuyajadili kama wadau na hatimaye kuchukua hatua ya kutatua ikiwemo kusimamia matumizi ya fedha kwa kufuata miongozo, ubovu wa miundombinu na utoaji wa taarifa za fedha katika shule ambayo ni mambo ya kuyafanyia kazi na wadau wote ili kuwa na ustawi wa elimu.
Wadau wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) baada ya kupokea ripoti
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ndugu Jeremiah Lubeleje akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa kikao cha wadau wa elimu kilicholenga kupokea taarifa ya utafiti wa ufuatiliaji wa Rasilimali fedha za umma kwa shule 20 uliofanywa na Shirika la Haki Elimu kupitia mtandao wa marafiki wa elimu Masasi (MEMA) tarehe 13.07.2018
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa