Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe.Rachel Kassanda leo tarehe 17 Februari 2026 amezindua rasmi zoezi la upandaji wa miti kwa lengo la kuendelea kuhifadhi Mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Amewataka pia Wananchi kupanda miti kwa wingi, kuitunza na kuacha tabia ya kukata miti hovyo ili kulinda vyanzo vya maji, na kuboresha hali ya hewa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Shule mpya ya Sekondari ya Mlingula na Chikunja zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mhe.Kassanda amesema kuwa Wilaya imejiwekea mkakati wa upandaji wa miche ya miti kila mwaka na kupitia Halmashauri iwe imepanda miti milioni 1.5 ili kurejesha hali ya miti iliyopotea ambayo imesababishwa na baadhi ya Wananchi kuwa na tabia ya kukata miti hovyo kwa ajili ya matumizi ya kuchoma mkaa na kwa mahitaji ya kuni kwa biashara.

" Ili kuendelea kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya utunzaji wa Mazingira, sisi wana Masasi lazima
tuwe sehemu ya kutengeneza Masasi ya kijani na hili linawezekana kama tutashiririkiana katika zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali , Wananchi muwe na desturi ya kupanda miti kwani ni alama kubwa"

Amesema zoezi hilo litakuwa ni endelevu ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za kutunza na kuhifadhi Mazingira hivyo amewasisitiza Wakala wa Misitu Tanzania ( TFS) Wilayani Masasi kuendelea kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa upandaji wa miti isiyopungua mitano kwa kila kaya sanjari na kusambaza miche ya miti hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni na kuhakikisha wanaisimamia miti inapandwa na hasa katika msimu huu wa mvua za masika.

Aidha Mhe. Kassanda amehitimisha mazungumzo yake kwa kutoa rai kwa Wanafunzi kuhakikisha kila mmoja atambue analojukumu la kupanda miti na kuisimamia kikamilifu, ili iweze kuwaletea tija katika maisha yao na hususani wanapokuwa katika mazingira ya shule wanaweza kupata vivuli, matunda ( lishe) n.k

Jumla ya miche 3800 imepandwa ikiwemo miche ya Mipapai, Mipera na Mikongo, ambapo katika shule ya Sekondari Mlingula imepanda miti 1800 na Chikunja ikipanda miti 2000.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa