MADIWANI MASASI DC WAPITISHA MAPENDEKEZO YA RASIMU YA MPANGO WA BAJETI YA SHILINGI BILIONI
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani MMtwara jana tarehe 17, Februari 2026 limepitisha Mapendekezo ya Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo Halmashauri inakadiria kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 46.8 kutoka vyanzo vyake mbalimbali na kutoka katika ruzuku ya Serikali kuu.

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri uliopo Mbuyuni Masasi na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo mhe.Ismail Chilumba ambaye pia ni Diwani wa kata ya Chikundi ambapo pamoja na mambo mengine amehaidi kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani ili kuwezesha kutekelezwa kikamilifu miradi ya maendeleo ambayo imeainishwa katika vipaumbele muhimu kwenye mpango wa bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Aidha bajeti kuu ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2026/2027 imeongezeka kwa asilimia 1.01 na Mapato ya ndani yameongezeka kwa asilimia 1.07 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 .

Bw.Faraji Mandoa kutoka Idara ya Mipango na Uratibu Halmashauri ya Wilaya ya Masasi akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2026/2027 amesema katika kuandaa bajeti ya mwaka 2026/2027 yapo mambo muhimu yamezingatiwa ikiwemo ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kipindi cha mwaka 2025 - 2030, Sheria ya bajeti Na.11 ya mwaka 2015, Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, mpango wa Wilaya wa miaka mitano na sera za sekta mbalimbali.

Mambo mengine ni Malengo endelevu ya Maendeleo ya 2030, maelekezo na ahadi mbalimbali za viongozi wakuu wa kitaifa, kuanzisha Miradi ya kimkakati kwa ajili ya kuongeza Mapato ya Halmashauri, kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya mfuko wa Maendeleo Ya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Halmashauri pamoja na kujikita kwenye miradi inayolenga kuleta matokeo chanya yenye kugusa maisha ya Wananchi moja kwa moja pia imezingatia kukamilisha miradi viporo na kulipa madeni ya wazabuni kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya.

Hata hivyo kulingana na mwongozo uliotolewa vipaumbele vya bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa fedha 2026/2027 ni pamoja na

●Kuendeleza miradi ya kimkakati kwa ajili ya kuongeza Mapato ya Halmashauri kwa uendelezaji wa ghala la mazao mchanganyiko katika kata ya Lukuledi na Chiungutwa.
●Kuhimarisha na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kununua gari moja.
●Kuboresha vituo vya Afya viwili (Chikundi na Chikoropola, na kukamilisha Zahanati 2 katika vijiji vya Nantona na Mdenga).
●Kipaumbele kingine ni kuimarisha ulinzi na Usalama wa Raia na mali zao kwa kuendeleza vituo 2 vya Polisi katika Kata ya Chiwale na Mbuyuni.
●Kuboresha huduma za Mawasiliano na Jamii kwa kuendeleza Redio Jamii (Masasi Fm).
●Kuendeleza miradi ya kimkakati ili kuongeza mapato ya Halmashauri kwa kujenga / kuboresha stendi ya Mabasi/ Hiace katika kata za Nanganga na Mbuyuni.
●Kukamilisha vyumba vya Madarasa 46, nyumba 3 za walimu na vyumba vinne vya maabara.
● Kupunguza uhaba wa watumishi kwa kuajiri watumishi wapya 750 kwa kada za Biashara na uwekezaji 6, Michezo na Utamaduni 2, TEHAMA 1, Afya 354 , Elimu Msingi 131, Elimu Sekondari 130, Wahasibu wasaidiI 1, Kilimo na Mifugo 43, Ujenzi 9, Usimamizi wa Manunuzi 3, Maendeleo ya Jamii 5 na Utawala 40.
Amesema uhaba huo wa watumishi umetokana na kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma kama vile Shule, Zahanati na watumishi wengine kustaafu utumishi wa Umma.

Kwa upande wao baadhi ya Madiwani waliochangia mjadala huo wametaka uwepo wa Usimamizi madhubuti ya miradi ili kuharakisha kukamilika kwa wakati miradi hiyo kwa manufaa ya Wananchi.
18/02/2026
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa