Kwa muda mrefu wananchi wa masasi wamekuwa na tatizo la uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama hali inayosababisha wananchi hao kutumia muda mwingi kutafuta maji katika visima vya asili ambavyo sio salama badala ya kufanya shughuli za maendeleo
Kutokana na tatizo hilo, Serikali imekuwa ikiweka jitihada za kuhakikisha inawahudumia wananchi kwa kutatua kero zinazowakabili ikiwemo ya upatikanaji wa maji, ambapo imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani kwa kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Tanzania kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya tatu katika Mradi wa ajira ya muda (PWP) imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali inayoibuliwa na wananchi ikiwemo miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vinavyonufaika na mradi lengo ikiwa ni kwaajili ya kuongeza kipato kwa walengwa kwa kulipwa ujira baada ya kufanya kazi katika kipindi cha hari na kupata fursa na ari ya kushiriki shughuli za maendeleo.
Halmashauri ya wilaya ya masasi ni kati ya Halmashauri zinazotekeleza mpango wa TASAF III ambapo jumla ya vijiji 97 vinanufaika na mradi kwa kupata ruzuku lengo ikiwa ni kupunguza umasikini kwa wananchi kwa kuweza kumudu huduma za chakula, elimu na afya mahitaji ambayo ni ya msingi kwa mwananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali kulinda vyanzo vya maji, uchimbaji wa visima vya maji na upandaji wa miti kwenye vijiji vyao kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira.
Wananchi wa kijiji cha mwena katika halmashauri ya wilaya ya masasi mkoani mtwara ni kati ya wananufaika wa mradi wa PWP ambapo kupitia mradi huo wameondokana na shida ya maji ya muda mrefu baada ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa maji katika kijiji hicho kukamilika katika awamu ya kwanza kupitia Miradi ya Ajira za muda (PWP) kwa walengwa wa mpango wa kunusufu kaya masikini TASAF awamu ya tatu.
Kufuatia utekelezaji wa mradi huo wananchi wa kijiji cha Mwena wameipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa miradi ya ajira ya muda huo ambao wamesema licha ya kuinua kipato chao lakini umetatua shida ya maji kijijini hapo kupitia mradi wa kusambaza maji ulioanza kutekelezwa mwaka 2017 ambapo walifanikiwa kusambaza maji katika vitongo vyake kwa kuweka vituo saba vya kuchotea maji.
Akiongea kwa niaba ya walengwa wengine Mtendaji wa kijiji Kelvin Milanzi alieleza kuwa walengwa wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini pamoja na wananchi wa kawaida waliamua kuibua mradi huo wa kusambaza maji kwenye vitongoji vyao kutokana na wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji wakati kuna miundombinu ambapo kazi iliyokuwa imebaki ni kuchimba mitaro na kulaza mabomba ili watu wapate maji
“Mradi unalenga kuwaongezea kipato wananchi masikini katika kijiji hiki kwa kufanya kazi kwenye mradi tulioibua lakini mradi baada ya kukamilika unanufaisha wananchi wote ,hivyo pamoja na kwamba tumeongezewa kipato lakini pia wananchi tunapata maji” alisema Kelvin.
Kwa upande wake ndungu Esha Elifa Salum ambaye ni mnufaika wa mradi wa kunusuru kaya masikini alisema uwepo wa miradi ya ajira ya muda katika kijiji cha mwena umeisaidia jamii nzima kwa kuwezesha upatikanaji wa maji huduma ambayo ilikuwa haipatikani kwa urahisi japo kuwa walengwa wamepata faida mara mbili kwa kuboresha maisha lakini pia kwa kupata huduma ya maji.
Usambazaji wa maji katika kijiji hicho cha mwena umegharimu shilingi 32,796,400 ambapo jumla ya shilingi 26,882,400 sawa na asilimia 75 zilitumika kulipa ujira kwa walengwa na shilingi 5,914,000 Sawa na asilimia 25 zilitumika kununua vifaa vya mradi kama mabomba koki na vitu vingine.
Mpango wa TASAF III ni kuwatoa watanzania katika hali ya umaskini kwa kuwapa ruzuku itakayowasadia kupata huduma muhimu ikiwa ni pamoja huduma za afya, kuwasaidia watoto wao waweze kwenda shule lakini baadhi ya wanufaika wamekuwa wakitumia fedha hizo kulewa badala ya kuanzisha miradi midogo midogo kama ufugaji wa kuku, mbuzi na kondoo pamoja na kilimo ili miradi hiyo iwasaidie kuwaongezea kipato
Jumla ya kaya 10,570 zilibainishwa katika vijiji 97 vya Halmashauri ya wilaya ya Masasi ambapo kaya hizo kaya 3,068 zimejiunga na mfuko wa afya ya jamii(CHF) nakuziwezesha kaya hizo kupata huduma ya afya kwa gharama nafuu ambapo watu sita wa kaya moja wanalipia elfu kumi tu (10000) kupata huduma za afya kwa kipindi cha mwaka mzima kwenye mamlaka ya utekelezaji husika.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa