Chama Kikuu Cha Ushirika MAMCU LTD Leo tarehe 05/08/2024 kimetoa ruhusa kwa Vyama vya Msingi (AMCOS) kuanza kukusanya mbaazi (kupokea) Kutoka kwa Wakulima huku wakihaidi Siku chache zijazo itatolewa ratiba kamili ya minada.
Aidha, viongozi hao pia wametakiwa kuzingatia kulinda ubora wa mazao hayo ambayo wanayapokea kutoka kwa wakulima kwani ubora wa mazao ndio upana wa Soko.
Hayo yameelezwa na Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Masasi Bw. Ahmad S.Issa katika kikao kazi cha kupitia zile changamoto ambazo wamekutana nazo wakiwa wanafanya jukumu lao la Msingi katika ukusanyaji wa zao la Ufuta na Kutoa fursa kupitia changamoto hizo sasa zitumike kwa namna bora ya kuelekea katika ukusanyaji wa zao la mbaazi, kikao kilichowakutanisha kwa pamoja viongozi wa AMCOS wa Halmashauri ya Wilaya Masasi yaani wenyeviti na makatibu, Afisa kilimo, pamoja na Afisa mapato, kikao kilichofanyika Katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo Mbuyuni Masasi.
Amesema" Leo tarehe 05/08/2024 tumepata kauli kutoka kwa meneja wa Chama kikuu Cha MAMCU LTD kwamba wameruhusu vyama vya Msingi vianze kukusanya mbaazi yaani kupokea Kutoka kwa Wakulima na siku chache mbeleni watatoa ratiba kamili ya minada, hivyo niwaombe wakulima hakuna haja ya kuuza mbaazi zao kwa walanguzi( (chomachoma) kwani maslahi makubwa tunayapoteza".
Amesema katika kutekeleza hayo wamekubaliana kuzingatia zaidi viwango vya ubora katika ukusanyaji wa mazao na itakapotokea kiongozi mmoja wapo haendani na taratibu zinazotakiwa wasisite Kutoa taarifa kwa Maafisa Ushirika au kwa kiongozi yeyote wa Serikali kujulisha tukio hilo hususani katika kulinda ubora wa mazao yanayotoka katika Halmashauri ya Wilaya Masasi.
"Pia tumesisitiza juu ya utumiaji wa ghala la Halmashauri ambalo lipo katika Kijiji Cha Chiungutwa, na hapa hususani katika Vyama vya Ushirika vyote 28 vinavyopatikana katika Jimbo la Lulindi kwasababu upatikanaji wa ghala hili ni mkombozi kwa Wakulima litawapunguzia gharama za usafirishaji wa Mazao hayo kutoka katika eneo la Chama chake cha msingi kupeleka maghala makuu ambayo yapo mbali na maeneo yao, hivyo viongozi hao wa vyama vya Ushirika wamelipokea vizuri japo Kuna maombi machache wameyatoa ikiwemo kuongezwa kwa wachukuzi katika ghala hilo ili kusiwe na msongamano kwenye suala la ushushaji wa mizigo na huduma zingine ziende kwa haraka.
Halmashauri ya Wilaya Masasi inajumla ya vyama 55 vya Ushirika,kilimo na masoko ambapo katika Jimbo la Lulindi vyama 28 na Jimbo la Ndanda likiwa na vyama 27.
05 August 2024
......@ Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa