Wataalamu Kutoka Hamashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Leo julai 09/2024 wamekutana na kuwajengea uwezo Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari ambao tayari Shule zao zimepokea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo na huku wakiwasisitiza kutumia mfumo mpya wa ununuzi wa umma wa kielektroniki (NeST)ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa umma (PPRA)
Matumizi ya mfumo huo pamoja kuwa ni maagizo ya Serikali pia ni matakwa ya sheria yaliyobainishwa Katika sheria mpya ya ununuzi wa sheria no.10 ya mwaka 2023.
Bw. Said Ally ni Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya Masasi akitoa ufafanuzi zaidi juu ya mfumo huo mbele ya walimu hao amesema "tumeamua kukutana na hawa walimu ili kuwajengea uwezo na kuwafahamisha Katika mapokezi ya fedha;walizopokea nini wanatakiwa kufanya kwenye fedha hizo."
Amesema Sheria mpya ya manunuzi inataka taasisi zote za umma kufanya manunuzi kupitia mfumo wa NeST ambao ni rahisi kutumia na unaondoa tabia za urasimu iliyokuwa ikijitokeza kipindi Cha nyuma, ukilinganisha na ule wa awali wa TANePS ambao ulikuwa na changamoto mbalimbali Kama vile uahirikishwaji ulikuwa mdogo sana na uliruhusu baadhi ya utaratibu kufanywa nje ya mfumo huo.
"Kwasasa ni kosa la jinai kufanya manunuzi ya umma nje ya mfumo wa kielektroniki (NeST) na kanuni ya 128 inatoa adhabu kwa mtu yeyote ambaye atafanya ununuzi kwa nje ya mfumo huo ambapo adhabu inaweza kuwa kulipa shilingi milioni 10, au kifungo Cha Miaka mitatu (3) jela.au vyote kwa Pamoja."
Aidha Bw. Said ameongeza kuwa kwasasa sheria inasema pia iwapo ununuzi wa nje wa mfumo wa kielektroniki utasababisha hasara yeyote au upotevu wa mali za umma,basi yule aliyehusika atahusika kulipa upotevu wa hasara hiyo.
Hata hivyo ifahamike kuwa sheria ya ununuzi wa umma imebadilika Kutoka kwenye Sheria ya mwaka 2011 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2016, ambapo Serikali iliamua kufanya maboresho mbalimbali kwenye hiyo sheria, kwaiyo kupitia sheria mpya no.10 ya mwaka 2023 kifungu no.73 imeondoa mwanya Moja kwa Moja wa kufanya manunuzi nje ya mfumo wa kielektroniki tofauti na ile sheria ya Mwanzo ambayo ilikuwa ikiruhusu manunuzi kufanywa kwa mfumo wa kielektroniki au nje ya mfumo huu.
Kikao hicho cha kuwajengea uwezo walimu hao kimeshirikisha Wataalamu Kutoka Idara ya mipango, Idara ya Fedha, Idara ya ujenzi, Idara ya ununuzi pamoja na kitengo Cha ukaguzi wa Ndani.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa