Imeandaliwa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Bi.Beatrice Claver Mwinuka amekabidhi rasmi Ofisi kwa Mkurugenzi mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Ndg.Alphaxard Mashauri Etanga.
Makabidhiano hayo yamefanyika Leo tarehe 11/02/2025 katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo Mhe.Ibrahimu Chiputula ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mpeta, huku baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo nao wameshiriki.
Awali akizungumza kwenye makabidhiano hayo Bi.Beatrice Mwinuka ameendelea kumshukuru mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumteua tena kwenda kuiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na kwamba kwa uzoefu alioupata wakati akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi anaimani kubwa anakwenda kuivusha Kilosa kwa Maendeleo zaidi.
Vilevile pamoja na kutumia nafasi hiyo kumkaribisha Mkurugenzi mpya wa Halmashauri hiyo Ndg.Alphaxard Etanga pia amewashukuru Watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi pamoja na Baraza zima la Madiwani kwa ushirikiano mkubwa waliompatia kwa kipindi chote alichohudumu katika Halmashauri hiyo na kwamba yupo tayari kutoa ushirikiano pindi watakapohitaji mawazo yake, na wao pia waendelee kumpa ushirikiano kama walivyokuwa wakimpatia yeye.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Ndg.Alphaxard Etanga pamoja na kumshukuru mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, pia amehaidi kushirikiana na timu yake ya Wataalamu pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri kuendeleza kile ambacho yeye amekifanya ili kuona Halmashauri ya Wilaya ya Masasi inaendelea kupiga hatua kimaendeleo kupitia Miradi ambayo inatekelezwa.
"Mimi nikuombe Bi.Beatrice kwamba nimepokea taarifa hizi ambazo umenipa, nitazipitia kwa kina,nitashirikiana na timu yangu ya Wataalamu pamoja na Mwenyekiti wetu wa Halmashauri na baada ya hapo tutaendeleza kila kizuri ambacho umekifanya, tunatambua kwamba umefanya kazi kubwa kwa kipindi kifupi, kuna Miradi ambayo umeitekeleza na kuanzisha mimi nakuhaidi nitaiendeleza"....alisema Ndg.Etanga
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Ibrahimu Chiputula akizungumza kwa niaba ya Baraza la Madiwani amesema, wana Masasi bado wataendelea kumkumbuka Mwinuka kwa mazuri aliyoyafanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na hivyo wanamuombea kwa Mwenyezi Mungu kheri na afya njema kwenye majukumu mapya ya kazi.
"Wape salamu Kilosa, tunaamini yale mazuri uliyotufanyia huku basi tunatamani ukawafanyie wanakilosa, nakushukuru tumefanya kazi kwa ushirikiano "
Pia Chiputula akahitimisha kwa kumkaribisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Mkurugenzi huyo mpya Ndg.Alphaxard Mashauri Etanga na kumueleza kwamba wana Masasi wanamatumaini makubwa kutoka kwake hivyo washirikiane katika kuijenga Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na wanatamani yale mazuri yanayoonekana katika maeneo mengine yapatikane katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
"Nakukaribisha, unatimu ya Menejimenti, utakuwa pia na Madiwani hivyo karibu sana tufanye kazi ili tuivushe Halmashauri yetu katika viwango".
Ikumbukwe kuwa tarehe 24 /01/2025 mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi kwa baadhi ya Viongozi mbalimbali, na katika uteuzi huo Ndg Alphaxard Etanga alikuwa ni miongoni mwa walioteuliwa na kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi huku Beatrice Mwinuka akihamishwa na kupelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro .
11/02/2025
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa