Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Leo tarehe 29/08/2024, limeketi na kupokea taarifa za fedha Kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni 2024.
Kwa mujibu wa kifungu Na.40 cha sheria ya fedha za Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982, pamoja na agizo katika kanuni za fedha za Serikali za Mitaa Na.31(the local authority Financial Memorandum of 2009) zinaeleza halmashauri zote nchini kufunga mahesabu yake ya mwisho wa mwaka na kuwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kabla au ifikapo tarehe 30 Agost ya kila mwaka.
Pia kupitia kanuni au mwongozo wa fedha za Serikali za Mitaa (LAFM) 2009 Na.31, taarifa ya mahesabu hayo yanapaswa kuwasilishwa katika Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango na hatmaye kwenye Baraza la madiwani kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na ndipo hesabu hizo kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali.
Bw.Joseph Maduhu ni muhasibu Halmashauri ya Wilaya Masasi awali akisoma taarifa hiyo ya fedha za mwisho wa mwaka kwenye Kamati ya Fedha uongozi na Mipango na hatmaye mbele ya baraza la Madiwani amesema hesabu za Halmashauri za kuishia juni 2024 zimefungwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya utayarishaji wa hesabu za umma pamoja na Kanuni za Fedha za Serikali za Mitaa.
Amesema katika hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi za kuishia juni 2024 mizania (statement of Financial Position) inaonyesha hali halisi ya Halmashauri kwa tarehe 30 Juni 2024.
Amesema " Halmashauri ilimaliza mwaka wa fedha 2023/2024 tarehe 30 Juni 2024 ikiwa na albaki ya jumla ya shilingi Bilioni 4,063,544,626.00 katika akaunti zake za BoT, CRDB na NMB pamoja na akaunti za Shule, Vituo vya Afya, zahanati na Vijiji"
"Pia Halmashauri ilikuwa inadai jumla ya shilingi 534,649,716.67 toka Katika taasisi mbalimbali na Watumishi kwa mchanganuo ufuatao:
*Mikopo vikundi vya Wanawake na Vijana shilingi 458,481,606.57
*Wadaiwa wa ushuru wa korosho (Vyama vya Msingi) sh.76,168,110.00
Aidha Bw.Maduhu ameongeza kuwa, Halmashauri imefunga mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwa na vifaa mbalimbali vilivyoko stoo kama vile madawa,shajala vyenye thamani ya sh.960,169,154 huku mali za kudumu kama vile Ardhi, majengo ya Ofisi, majengo ya makazi, majengo ya zahanati, Vituo vya Afya, hospital, Shule, Magari, pikipiki, mitambo n.k zikiwa na thamani ya sh.48,048,565,315 .
"Kwa mwaka 2023/2024 Halmashauri imejenga na kununua mali za kudumu zenye jumla ya shilingi 4,652,701,189.00 ambazo zimenunuliwa kwa ruzuku toka Serikali kuu Pamoja na fedha za mapato ya ndani."
Hata hivyo Bw.Maduhu katika taarifa hiyo amehitimisha kwa kusema kuwa Halmashauri pamoja na kuwa na hisa katika kampuni ya majani ya chai (TATEPA) na mtaji mwingine katika Bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa, kulingana na taarifa ya mwenendo wa fedha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya utayarishaji wa hesabu mapato yalifikia sh.44,259,839.00 na matumizi sh.33,422,883,885.00 hivyo kufanya ziada ya sh.10,836,955,504.00 Kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30/06/2024.
Nao kwa upande wao waheshimiwa Madiwani baada ya kupokea na kujadili taarifa hiyo na hatmaye kuipitisha, wote kwa Umoja wao wameonyesha kuridhishwa na namna ambavyo imeandaliwa taarifa hiyo Kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya utayarishaji wa hesabu.
Baraza hilo la madiwani la kupokea taarifa za ufungaji wa mahesabu ya fedha za mwisho wa mwaka limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo uliopo mbuyuni Masasi huku likiwashirikisha Madiwani, Wakuu wa Idara na vitengo, Viongozi wa vyama vya Siasa, Maafisa Tarafa, Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya Pamoja na wadau wengine.
29/08/2024
@... Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa