Halmashauri ya Wilaya Masasi imeendelea kunufaika na Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo tarehe 30 June 2023/2024 katika mwisho wa mwaka wa fedha Rais Dokta Samia Suluhu Hassan aliipatia fedha Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kiasi cha Shilingi Milioni 560,552,827, na Halmashauri ililazimika kuvuka nazo katika mwaka mpya wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali.
Halmashauri ilianza kutangaza tenda na hatmaye kumpata mkandarasi ambaye alikubali kuifanya kazi hiyo Kwa moyo mmoja Lakini siku chache tu mkandarasi huyo akaamua kuiacha kazi hiyo kwa ridhaa yake mwenyewe, na ndipo Halmashauri ikachukua hatua za haraka kutangaza tenda kwa mara Nyingine na kubahatika kuipata kampuni ambayo ilianza utekelezaji wa mradi huo mara Moja.
Hata hivyo Kasi ya utekelezaji wa mradi huu imeelezwa kuwa bado ulikuwa ni wakusua sua kutokana na kampuni kubainika kuwa na vibarua vingi katika maeneo mengine tofauti na mradi huu na ndipo sasa Halmashauri ililazimika kuuvunja mkataba na kuamua Sasa kuutekeleza mradi huu kwa kutumia mafundi wa kawaida (force account).
Mradi huu ambao unatekelezwa kwa fedha za Sequip unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi January 2025 umeanza tena utekelezaji wake mapema November 2024 huku ukijumuisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 8 huku kila Jengo likiwa na Ofisi katikati yake, Jengo la utawala 1, Jengo la maabara ya kemia na Biolojia, Nyumba ya mwalimu (single) Maktaba, Chumba Cha Tehama, Vyoo vya wanafunzi matundu 4 (wav) Vyoo vya wanafunzi matundu 4 (was) kichomea taka pamoja na Tanki la Maji ya Ardhini.
Bw.Shaban Kinyongo ni Afisa Elimu vifaa na Takwimu Halmashauri ya Wilaya Masasi ameeleza kwamba mradi huu unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo katika awamu hiyo ya pili mradi utapata mabweni kwa ajili ya kulala wanafunzi pamoja na bwalo " kwaiyo tunasubiria baada ya awamu hii ya Kwanza kukamilisha mradi, tutapata fedha nyingine katika kuendeleza mradi huu, hivyo nasisitiza mafundi waongeze Kasi katika ujenzi ili ifikapo January mwishoni iwe imekamilika na tuanze usajili wa wanafunzi katika Shule hii ya Amali ambayo ni mpya Katika Halmashauri yetu"..alisema bw.Kinyongo
Ameongeza kuwa malengo na matarajio ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na Serikali kwa ujumla mara baada ya kumalizika kwa ujenzi wa Shule hii ya Amali na Wanafunzi kuanza kunufaika na Elimu itakayotolewa kutaimarisha, kupanua na kuendeleza uwelewa kwa kina wa maarifa, stadi na mwelekeo alioupata katika hatua ya Elimu ya Msingi.
Kukuza stadi za ufundi na ujasiriamali zitakazo mwezesha kujiajiri, kuajiriwa na kuyamudu maisha kwa kutumia vizuri mazingira yake,"shule hii itazalisha Wataalamu wengi sana"
Kuimarisha mawasiliano kwa kutumia stadi za lugha, kukuza tabia ya kujiamini na uwezo wa kujifunza kwenye nyanja mbalimbali zikiwemo sayansi na teknolojia, maarifa ya kinadharia na ufundi, kuimarisha uwajibikaji katika masuala mtambuka ya Jamii yakiwemo Afya, usalama ,usawa wa kijinsia na utunzaji endelevu wa mazingira.
Kukuza utayari wa kujiendeleza na mafunzo ya Elimu ya amali na sanifu au Sekondari hatua ya juu.
Hata hivyo Bw.Kinyongo pamoja na kuwakumbusha wanafunzi waendelee kusoma kwa bidii Lakini pia amewasisitiza wazazi/walezi kuwaandaa vizuri Watoto wao ili wajiunge na shule hiyo ambayo itakuwa ni chachu kwa Maendeleo Yao hapo baadaye baada ya kuhitimu na kupata cheti kitakacho onyesha taaluma-aliyosomea lakini watapata ujuzi wa kudumu ambao utawawezesha kujiari au kuajiriwa.
Shule hii ya Sekondari ya Amali ambayo inajengwa katika Kijiji Cha mbuyuni kata ya mbuyuni Halmashauri ya Wilaya Masasi ikikamilika inatarajia kusajili Watoto takribani 400 kwa mkupuo mmoja ( Madarasa 8 @wanafunzi 50) na huku ikitoa uwanja mpana wa kuimarisha uwezo wa mwanafunzi katika stadi za vitendo ili kuwapa maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kisasa.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa katika kuhakikisha Elimu ujuzi vinachukua nafasi Serikali imeanzisha mtaala wa Elimu ya amali, hasa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka mageuzi kwenye mfumo wa Elimu .
Rais Dkt. Samia ndiye aliyeanzisha mjadala wa kitaifa aliagiza kufanyike Mapinduzi ya mfumo wa elimu nchini na hatmaye Watendaji wake wakaanza kuingia kazini na kufanya maboresho ya mtaala wa Elimu ya Msingi na Sekondari.
Shukrani.
Halmashauri ya Wilaya ya Masasi inaendelea Kutoa shukrani za dhati kwa mhe.Rais Dokta Samia Suluhu Hassan Kwa kutupatia Fedha kiasi cha shilingi Milioni 560,552,827 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Amali ambayo inajengwa katika Kijiji Cha mbuyuni kata ya mbuyuni Halmashauri ya Wilaya Masasi.
Na: Kitengo Cha Habari na Mawasiliano (H/W) Masasi.
24/12/2024
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa