Wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya Halashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara, wametakiwa kutoa huduma bora kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao ili kupunguza vifo mama na mtoto vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Agizo hili limetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bibi Changwa Mkwazu wakati wa kufungua kikao kazi kwa watumishi hao kilicholenga kufanya tathmini ya mpango kazi wa utoaji huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kila mwezi na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza ili kuboresha utoaji wa huduma hizo.
Mkurugenzi Mkwazu amewaeleze wakuu wa vituo hao kuwa, kwa mjibu wa taarifa ya Mkoa hali ya utoaji wa huduma, imeonesha kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu vifo 9 vya wajawazito wakati wa kujifungua na vifo 73 vya watoto chini ya miaka mitano vimeripotiwa kutokea katika halmashauri hiyo na kusababisha halmashauri kushika namba moja kati ya halmashauri 9 za mkoa huo.
Mkwazu amesema kuwa “inaumiza sana kumpoteza mama au na mtoto wakati wa kujifungua wakati tungeweza kuzuia baadhi ya vifo hivyo kwa kutoa rufaa mapema , kutoa elimu ya uzazi salama na mengine mengi, hivyo , hizi takwimu za vifo sio nzuri hata kidogo, tekelezeni wajibu wenu ipasavyo”
Aidha Mkurugenzi amewakumbusha wakuu wa vituo hao, kutoa elimu ya Uzazi salama kwa wajawazito ikiwemo umuhimu wa kuhudhuria kliniki, kula mlo kamili (lishe) pamoja na kuwapima vipimo stahiki ikiwemo kipimo cha uwingi wa damu ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na masuala hayo.
Pia Mkwazu amesema “Nawaagiza wakuu wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya ambavyo havina mashine ya kupima uwingi wa Damu vinunue haraka iwezekanavyo kwani kuna vifo vingine vinasababishwa na mama mjamzito kutokuwa na damu ya kutosha wakati wa kujifungua”
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Bibi Miriam Cheche amesema kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya mkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeongoza kuwa na vifo vingi vya mama na mtoto ambapo vifo 8 kati ya 9 vilitokea Hospitali ya Rufaa Ndanda na kati ya watoto 73 walifariki, vifo 33 vilitokea kituo cha afya Nagaga
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Bibi Miriam Cheche akitoa maelekezo kwa wakuu wa vituo vya kutolea huduma leo tarehe 20.08.2020 kwenye kikao kazi cha tadhimini ya utoaji huduma kwa miezi mitatu iliyopita
Cheche ameeleza kuwa “sababu kubwa iliyopeleka Hospitali ya Rufaa ndanda na kituo cha Afya Nagaga kuwa na vifo vingi ni kutokana na kuhudumia watu kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Halmashauri lakini tutajitahidi kuongeza umakini na ubora katika kutoa huduma zetu kwa wagonjwa hasa wajawazito “
Aidha Kaimu Mganga Mkuu huyo amewasisitiza wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya kutoa rufaa ya kwenda hospitali kubwa kwa haraka pale mama mjamzito anapokuwa na changamoto ya kujifungua kwenye kituo chake.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa