Benki kuu ya Tanzania (BOT) Tawi la Mtwara leo tarehe 05/09/2024 imetoa Elimu ya namna bora ya utunzaji wa noti pamoja na utambuzi wa alama muhimu za usalama katika noti za Tanzania kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.
Lengo ni kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanazifahamu alama hizo za usalama ili kuepukana na fedha bandia ambazo zimeanza kupanda kasi katika mzunguko wa kifedha.
Pia washiriki wamejifunza kuhusu historia ya kifedha nchini na mchakato wa utengenezaji wa noti ambao kwa asilimia kubwa fedha inayotengenezwa inatokana na mahitaji.
Bw.Melchiades Rutayebesibwa ni Meneja huduma za kibenki tawi la Benki kuu Mtwara ambaye ndiye mwezeshaji wa mafunzo hayo amesema kwamba wamekuja hapo Halmashauri mahususi kuwapa elimu wafanyakazi wote waweze kuzitambua fedha zao na kwamba alama hizo zipo upande gani, lakini pia wakitoka hapo wakawe mabalozi wazuri wakuelimisha Jamii kuhusu umuhimu wa kuziheshimu na kuzitunza vizuri noti zetu kama alama ya utaifa wetu.
Amesema "ni muhimu kwa wananchi kuzitambua alama halisi zinazopatikana kwenye noti halali za Tanzania ili kuepuka utapeli wa kupewa noti bandia na hasa katika kipindi hiki cha ununuaji na uuzaji wa mazao na pia mifugo kutoka kwa Wakulima na Wafugaji."
Ameongeza kuwa ni vyema Sasa wafanyabiashara wakawa na vifaa maalumu vinavyoweza kutambua noti halali na bandia ambapo ni pamoja na taa maalumu zenye mwanga wa zambarau (Utraviolet light bulb) kwa kuwa taa hizo zina uwezo wakutambua alama muhimu zilizo katika noti halali ambazo si rahisi kuzitambua kwa macho ya binadamu pasipo vifaa hivyo.
Kwa upande wa utunzaji wa noti za Tanzania Watumishi hao wameshauriwa kuzingatia utunzaji bora wa noti hizo kwa kuepuka kuzishika katika hali ya unyevu unyevu, kuzikunjakunja au kufinyanga mkononi, wasihifadhi kwa kuchimbia ardhini, kuweka noti kwenye nguo za ndani au kuzifunga kwenye kanga, wasiweke noti kwenye soksi, viatu, chini ya godoro, n.k
Hata hivyo Bw. Rutayebesibwa amehitimisha kwa kuendelea kuwaomba Wananchi hasa wafanyabiashara wakubwa na wanunuzi wa mazao kutopendelea kupokea fedha taslimu mkononi badala yake watumie njia za kibenki na huduma zingine za kifedha kama vile Airtel money, M-Pesa, Tigo pesa, Halo -pesa na zingine nyingi tu ili kuepuka kuchomekewa fedha bandia au kuporwa.
05/09/2024
@.. Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa