UJIO WA MWENGE WA UHURU MASASI KUMULIKA UWEKEZAJI KATIKA ELIMU
Posted on: June 5th, 2018
Ujio wa mwenge wa uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara utakaopokelewa na kukimbizwa tarehe 13 juni, 2018 , unatarajia kuona kwa vitendo uwekezaji katika elimu kwa kupitia miradi ya miundombinu na jinsi jamii inavyoshiriki katika kuboresha elimu kwa kutoa chakula mashleni na kujenga miundombinu kama madarasa lengo ikiwa kufanya mazingira ya kufundishia na kujifunzia kuwa mazuri na hivyo kuinua ufaulu.
Akiongea ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi Changwa M. Mkwazu alisema, Mwenge wa uhuru ukiwa Masasi utakimbizwa kwenye vijiji 18 kata 8 na tarafa 3 na utapokelewa katika kijiji cha Mpeta na kukimbizwa katika Vijiji vya Chiungutwa, Ndwika, Nagaga, Namombwe, Mkwaya na utakesha katika kijiji cha Mnavira kata ya Mnavira ambapo katika miradi hiyo miradi ikiwemo ya elimu iliyotekelezwa kwa fedha za serikali na nguvu za wananchi itawekewa mawe ya msingi .
Mkwazu alieleza kuwa kwa ujumla, Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri hiyo, utaweka mawe ya msingi katika miradi minne (4) , kuzindua klabu ya wapinga rushwa na kugawa hundi za mikopo kwa vikundi 41 vya wananwake na vijana zenye thamaani ya shilingi milioni 144,219,000.
Mkurugenzi aliendelea kueleza kuwa, Kama ujumbe na kauli mbiu ya mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2018 unalenga kuwekeza katika elimu, halmashauri ya wilaya ya masasi imeendelea kutekeleza kwa vitendo kwa kujenga miundombinu na kutoa elimu kwa jamii juu ya kushiriki katika kuboresha elimu ikiwemo kuchangia chakula ili wanafunzi kupata chakula cha mchana.
Akifafanua juu ya miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru Mkurugenzi alisema, Miradi itayowekewa mawe ya masingi na Mwenge wa Uhuru ni mradi wa ujenzi wa madarasa 7, maabara 1 mabweni 2 na jengo la utawala 1 katika shule ya wasichana ndwika unaoghalimu shilingi milioni 400, ujenzi wa majengo ya wodi 1, chumba cha upasuaji 1,maabara 1, mochwari 1 na nyumba ya mtumishi 1 katika kituo cha Nagaga unaogharimu shilingi 400, mradi wa maji makong’onda –rivango unaogharimu shilingi bilioni 1,415,000,000, ujenzi wa madarasa 3 shule ya msingi Mnavira unaogharimu shilingi milioni 26,000,000 kwa nguvu ya wananchi na halmashauri na hundi za mikopo kwa vikundi 41 vya wanawake na vijana zenye thamani ya shilingi milioni 144,219,000
Hivyo Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 utapitia miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 2,385,219,000 Alisema Mkwazu.
Kuhusu Ujumbe na Kauli mbiu ya Mbio Za Mwenge wa Uhuru 2018 inayosema “UWEKEZAJI KATIKA ELIMU” chini ya kauli mbiu inayosema “ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA, WEKEZA SASA” Mkwazu ameeleza kuwa halmashauri inatekeleza kwa vitendo kwani elimu imeendelea kuboreshwa kimiundombinu lakini pia jamii imeendelea kuelimishwa juu ya dhana ya Elimu bila Malipo ambapo wazazi wamehamasika kuchangia na kusimamia zoezi la utoaji wa chakula mashuleni na kujenga miundombinu kama madarasa lengo ikiwa ni kuongeza ari ya wananfunzi kupenda shule na hivyo kuinua ufaulu.