Tarehe 29.07.2020 Rais mstaafu wa Tanzania awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa amezikwa kijijini kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara baada ya kufariki dunia tarehe 24.07.2020 kwa mstuko wa moyo akiwa hospitali jijini Dar es Salaam alikokuwa anatibiwa ugonjwa wa Malaria.
Katika mazishi hayo, Mamia ya waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali ya wilay ya Masasi na mikoa jirani walijitokeza kuuaga mwili wa rais huyo kwa kutoa heshima za mwisho kabla ya kumzika katika makaburi yaliyopo nyumbani kwake kijiji cha lupaso alikozaliwa.
Wananchi wakifuatilia shughuli ya Mazishi ya Rais mstaafu wa Tanzania awamu ya tatu, Benjamin William yaliyofanyika nyumbani kwake Lupaso
Mazishi hayo yamehudhuriwa na Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli pamoja na marais wastafu Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi, ambao wamemsifu kiongozi huyo kwa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa hilo, kupitia nafasi mbalimbali alizozishikilia.
Katika shughuli ya mazishi hayo Mhe. Rais wa Tanzania John Magufuli amewataka watanzania waendelee kumuombea Hayati Rais Mkapa na kuwasisitiza kuiga tabia zote njema alizokuwa nazo wakati wa uhai wake ikiwa pamoja kuwa mzalendo wa kweli na kupenda nyumbani kwao.
Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli ( wa kwanza kushoto)pamoja na marais wastafu Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi akitoa heshima baada ya kuweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati Benjamin Mkapa
Magufuli amesema Mkapa aliyaishi maisha yenye upendo wa kweli na alipenda nyumbani kwao kwani hata pale serikali ilivyojaribu kutenga eneo maalumu la kuzikia viongozi wa kitaifa jijini Dodoma alipinga wazo hilo na kuagiza atakapofariki azikwe kijijini kwao kwenye makaburi ya familia.
Kwa upande wake Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, amemuelezea Hayati Benjamin Mkapa kama kiongozi aliyechukia nchi na watu wake kuwa maskini na kulipa kipaumbele suala la uchumi kwa kuanzisha dira ya taifa ya kufikia uchumi wa kati ifakapo mwaka 2025 na pato la mtanzania kufikia dola 3000.
Kikwete alifafanua kuwa “Niliendeleza sera hiyo katika uongozi wangu na kwa sasa Rais Wetu wa awamu ya Tano anaendelea nayo ambapo sasa Tanzania ni moja ya nchi zenye uchumi wa kati, tunaenda vizuri”
Ameongeza kuwa Hayati Benjamin Mkapa alikuwa kiongozi mwenye utambuzi na manufaa kwa wananchi wake kwa kuwa alipenda kusikiliza, kushughulikia changamoto na kutoa mrejesho.
Akizungumza katika shughuli ya mazishi ya Mkapa, rais mstaafu wa awamu ya pili. Mzee Ali Hassan Mwinyi alisema hayati Benjamin Mkapa alikuwa mwanadamu na ana makosa yake kama wengine hivyo aombewe kwa Mwenyezi Mungu.
"Huenda alifanya makosa asiyopenda Muumba wetu, tumuombee msamaha kwa mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake, amuwie radhi, Mkapa alikuwa mtu mwema na mkrimu, asiependa masihara kwenye kazi," alisema Mwinyi.
Rais mstaafu wa Tanzania awamu ya tatu, Hayati Benjamin William Mkapa alizaliwa mwaka 1938 kijiji cha lupaso katika Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.
Viogozi mbalimbali wa Serikali wakiwa kwenye hafla ya Mazishi ya Benjamin Mkapa
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa