Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara wametakiwa kuwahamasisha wananchi wao kulima kilimo cha muhogo kinachotumia mbegu ya kisasa aina ya kiroba badala ya mbegu za asili ambayo inastahimili ukame na magonjwa lengo ikiwa ni kueongeza kipato na kuwa na uhakika wa chakula.
Viongozi hao walielezwa hayo kwenye warsha iliyoendeshwa na taasisi ya kimataifa ya kilimo inayojihusisha na utafiti wa masuala ya kilimo IITA kwa kushirikiana na MEDA na wizara ya kilimo iliyolenga kuwahamasisha viongozi hao kuweka mipango ya kuwekeza katika mbegu bora za muhogo ili kuweza kutosheleza mahitaji ya mbegu hizo kwa wakulima na kuongeza uzalishaji.
Akizungumza na viongozi hao ndugu Davis Mwakanyamale kutoka taasisi ya IITA alisema tafiti ya mbegu hizo ilikuja kwa ajili ya kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wakulima wa muhogo kwa kutumia mbegu bora za kisasa ambazo hazishambuliwi na magonjwa kwa kuwezesha upatikanaji wa mbegu hizo katika ngazi ya vijiji na kata badala ya kutegemea taasisi zinazozalisha mbegu pekee.
Mwakanyamale alisema kuwa mbegu za asili zinashambuliwa sana na magonjwa kama Batobato na Michirizi Kahawia hali inayopelekea uzalishaji wa zao hilo kutokuwa na tija, wakati mbegu ya kiroba ambayo inastahimili magonjwa, kuzalisha kwa wingi (tani 20-30 kwa hekta moja), zinakomaa kwa muda mfupi (Hukomaa miezi tisa tu baada ya kupanda) ukilinganisha na mbegu za asili ambazo pamoja na kushambuliwa na magonjwa lakini pia uzalishaji wake ni mdogo ambapo hekta moja inazalisha chini tani tano tu.
Mwakanyamale alisema kutokana na umuhimu wa zao la muhogo serikali imeliweka zao la Muhogo miongoni mwa mazao ya kipaumbele ya kuzalishwa kibiashara katika awamu ya pili ya mapango wa maendeleo ya sekta ya kilimo(ASDP) hivyo ni wakati mwafaka kwa halmashauri kuweka mkakati wa kuzalisha mbegu bora ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu hizo kwa wakulima.
Kwa upande wa mtaalamu kutoka taasisi ya MEDA inayojihusisha na utayarishaji wa mbegu bora za muhogo ndugu Erick Mwongolo alisema waheshimiwa madiwani ndio watakaosaidia kufikisha ujumbe wa hamasa kwa wakulima juu ya uzalishaji na matumizi ya mbegu bora za muhogo ili kutumia fursa hii kuongeza kipato na upatikanaji wa chakula wa wananchi wao.
Mihogo ya asili ni ile iliyoendelea kulimwa miaka mingi iliyopita na kurithiwa vizazi kwa vizazi. Mihogo hii ina sifa kadhaa ikiwemoHutoa mavuno wastani wa tani kwa Hekta, Mingi inachukua muda mrefu kukomaa, inahifadhika shambani kwa muda mrefu bila kuoza, hushambuliwa na magonjwa kama Ugonjwa wa michirizi ya ki-kahawia, batobato na blaiti, Hushambuliwa na wadudu milibagi na imezoeleka na wakulima hivyo wanaijua tabia yake na jinsi ya kuitunza.
Kuna zaidi ya aina 45 za mihogo zinajulikana nchini Tanzania. Zaidi ya asilimia 80 ya mihogo ni ya asili. Hivyo ni kusema wakulima wengi hawatumii mbegu bora. Ingawa wakulima wengi pia hupendelea kulima mihogo michungu kwa sababu haishambuliwi sana na wadudu ama magonjwa shambani na makopa yake yanahifadhika kwa urahisi, zaidi ya asilimia 70 ya mihogo ni mihogo baridi
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa