Katika kuelekea kilele Cha maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara kupitia Divisheni ya Maendeleo ya jamii imeendelea Kutoa Elimu kwa umma kwa kufanya vipindi vya Redio, midahalo na mijadala ya wazi Katika vijiwe vya boda boda, mashuleni, na vijijini Lengo likiwa ni kuwajengea uwelewa na kuwakumbusha wajibu na mchango wao Katika Maendeleo ya Familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza Katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika Leo tarehe 02 /05/2024 katika Kijiji Cha Mitonji, Kata ya Mbuyuni Halmashauri ya Wilaya Masasi Bw. Muhsini Kombo ambaye ni Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri hiyo amesema kwamba, kwa mujibu wa kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya wiki ya familia kwa mwaka huu yanasema Tukubali tofauti zetu kwenye familia, kuimarisha Malezi ya Mtoto, imelenga sana Moja kwa Moja kuijenga Familia yenye ubora kwa kutengeneza usawa wa familia iliyo na amani, upendo na kuziondoa zile tofauti mbalimbali ambazo zinajitokeza kwenye familia kama vile tofauti za kimawazo, kifikra, kipato, kitamaduni, kijamii n.k ambazo hizo ndio chachu ya kuzifanya familia zisiwe bora na kupeekea Malezi duni kwa Watoto na kutofikia mustakabali wa Familia n malengo yao kwa ujumla.
Amesema"tofauti hizi Sasa labda kuvunjika kwa ndoa, ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto kwasababu Watoto hawa pia wanaweza wakakosa haki zao za Msingi Kama vile kuishi, kusomeshwa, kupata Lishe Bora n.k, hivyo basi ili kujenga au Familia ipate Malezi bora lazima tuhakikishe tunakuwa wasimamizi wazuri kwa Familia bila kujali tofauti zetu, ambapo nina imani kubwa tukifanya haya sote kwa pamoja tutapata malengo chanya ambayo yatasaidia kufikia Malezi yaliyo Bora kwa Watoto wenu, kwani Watoto hawa tunaowalea Leo hii ndio Wazazi na Walezi wa family za kesho".
Aidha Bw.Kombo ameongeza kuwa, katika kutumia fursa ya wiki hii ya Familia hadi kilele chake ifikapo tarehe 15/05/2024 ni lazima tuendelee kuhamasishana uwelewa wa matatizo ambayo yanazikumba Familia kwa ujumla kutokana na Maendeleo ya kiteknolojia, utandawazi na mitandao ya kijamii ambapo Ndani ya familia lazima utakutana na watu wa ukweli wenye kuwa na Moyo wa upendo, ukarimu na mshikamano, kwasababu upendo unapokosekana Katika Familia ndio matatizo ya baadaye huzaliwa ndani ya familia, lakini pia hata uhusiano wa Jamii kwa maana familia ni Msingi na kiunganishi Cha familia na jamii yake inayomzunguka.
Amesema pia katika Familia ni mahali ambamo kila mmoja yupo na anapata mambo ya Kweli zaidi hivyo anapenda Sana kuwahasa watanzania kutenga muda wa kutosha kukaa na familia zao ili kujadili, kushauriana na kutekeleza masuala muhimu ya kuendeleza familia zao kwani familia Ndio kitovu Cha Maendeleo na pia kama Kuna Watumishi nao wanawajibu wa kutenga muda wa kazi na muda wa kushughulikia Familia zao ili kujenga maadili na Maendeleo ya Familia.
Ameendelea kwa kusema kuwa, "Familia nyingi za kitanzania zinakabiliwa na kuwepo kwa mila na desturi zenye kuleta madhara Kama umaskini uliokithiri , mawasiliano na miundombinu mibovu ambayo husababisha hali ya maisha ya Watu kuwa duni na tegemezi na hatmaye kutumia muda mwingi wa kufanya kazi bila kujali madhara yatakayotokea kwa familia.
Bi.Mariam Said na Hatib Idrisa ni baadhi ya Wananchi ambao wameshiriki mkutano huo, pamoja na kushukuru kwa kufikishiwa Elimu hiyo inayohusu Familia ambayo ni muhimu kwao na hivyo kuomba suala hilo liwe endelevu, pia wameiomba Serikali kutunga Sera na Sheria Kali kwa Wazazi ambao Mara nyingi wamekuwa wakienda kuolewa huku nyuma wakiwatelekeza Watoto wao na kupelekea kijilea wao wenyewe hali ambayo inawaweka Watoto hao katika mazingira magumu hususani kukosa ulinzi na Malezi bora.
Maadhimisho ya wiki ya familia yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na.47/257 la tarehe 20 Septemba 1993 linaloidhinisha kuwa na siku maalumu kwa ajili ya familia, na Tanzania ni Moja ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hivyo huungana na nchi Nyingine kila Mwaka kuadhimisha siku hii .
Kwa Mwaka huu maadhimisho haya kwa Mkoa wa Mtwara yatafanyika kimkoa katika Kijiji Cha Majengo Kata ya Ziwani Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Tarehe 15/05/2024 huku Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mhe.Kenan Patrick Sawala anatarajia kuwa Mgeni rasmi.
Imeandaliwa na Winifrida Ndunguru.
Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya Masasi.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa