Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu Optatus Lusolela, leo tarehe 26 juni 2025 amefungua Mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa utendaji kazi wa Taasisi (PIPMIS) na mafunzo ya mfumo wa Utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS).
Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yamefanyika katika ukumbi wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, uliopo Masasi mjini yamewakutanisha kwa pamoja Watumishi wa Umma kutoka Halmashauri ya mji Masasi pamoja na watumishi umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
Akizungumza wakati akifungua Mafunzo hayo Ndg. Lusolela amesema kwamba lengo kubwa la kutoa mafunzo hayo kwa Halmashauri zote mbili juu ya matumizi ya Mfumo wa kupima utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma ni kuendelea kuwajengea uwezo wa namna nzuri ya utumiaji wa mfumo huo na hatmaye waweze kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
"Serikali imetumia fedha nyingi baada ya kuona kuna Watumishi wamekosa stahiki zao, japo hapo awali kuna waraka ulitolewa kuwa tunapaswa kuanza kutekeleza mfumo huu wa utendaji kazi (PEPMIS), PIPMIS , kwaiyo niwaambie washiriki huu ni utekelezaji wa kisheria na ndio maana Serikali baada ya kuona huu udhaifu imewatoa Wataalamu wa Utumishi nchi nzima wanazunguka katika maeneo yetu na kutupa elimu hii, hili suala ni la umuhimu sana naomba tuwe na desturi ya kupitia miongozo ya mfumo huu wa Usimamizi wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma na tukifanya hivyo hatutakuwa na udhaifu katika mfumo huu " alisisitiza Lusolela
Ameongeza kuwa kwasasa kila kitu kinaenda kwa hatua mfano kuna uandaaji wa mpango,Ufuatiliaji wa utekelezaji, Uishaji wa mipango, tathimini ya utendaji kazi na masuala mengine hivyo amewaomba kusikiliza kwa umakini na kuyafanyia kazi yale yote ambayo wanafundishwa ili katika mwaka mpya ujao wa fedha unaoanzia mwezi julai 2025 watekeleze vizuri na weledi mkubwa hatmaye waendelee kuweka Utumishi wa Umma imara.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw.David Jeremiah Wembe amesema, wapo kwenye zoezi la kuwajengea uwezo wasimamizi, watumishi kwenye eneo la utendaji kazi katika mfumo.
"Kama kuna mtu yeyote au msimamizi alikuwa hajaelewa sehemu yeyote tumekuja kutoa elimu na ufafanuzi ili tuwe na uwelewa wa pamoja kwa maana mfumo huu umesha anza kuleta matokeo kwenye utendaji kazi wetu".
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia elimu ya namna nzuri ya utumiaji wa mfumo wa Usimamizi wa utendaji kazi (PEPMIS)na kwamba wamehaidi kuitumia vyema elimu hiyo ili kuepuka zile changamoto ambazo walikuwa wakikutana nazo wakati wanapotakiwa kuutumia mfumo huo.
Mafunzo hayo yamewashirikisha Wakurugenzi kutoka Halmashauri zote mbili, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa kata, Wakuu wa shule, Walimu wakuu na Wafawidhi .
26/06/2025.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa