Mpango wa usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri wa miaka mitano katika Halamshauri ya Wilaya ya Masasi unatarajia kusajili na kutoa vyeti bure kwa watoto 35,720 wanaoishi katika halmashauri hiyo ndani ya siku kumi na mbili (12) kuanzia tarehe 26 mwezi huu za kampeni ya usajili na utoaji wav yeti vya kuzaliwa kwa watoto hao.
Usajili huu wa vyeti vya watoto chini ya miaka mitano utatolewa katika ngazi ya kata na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia sasa badala ya ofisi ya mkuu wa wilaya ili kupunguza ghrama na usumbufu kwa wananchi kupata huduma hiyo hiyo .
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usajili wa watoto chini ya umri wa miaka 5 Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya masasi Chagwa M Mkwazu kwa watendaji wa kata wasimamizi wa vituo vya afya na waja leo katika ukumbi wa Migongo alieleza kuwa zoezi hilo ni muhimu sana hivyo wawezeshwaji watapaswa kuwa makini sana wakati wa utekelezaji ili kufikia lengo lililowekwa katika kipindi cha kampeni.
“Kuwasajili watoto hawa kutasaidia serikali katika ngazi mbalimbali kupanga mipango mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu kwa uhakika ikiwemo kujua mahitaji halisi ya madarasa, madawati, na hudma zingine katika jamii kulingana na idadi ya watu hivyo utoaji wa takwimu zisizosahihi zitaathiri upangaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa jamii”. Alisema mkwazu.
Mkwazu alieleza kuwa Cheti cha kuzaliwa ni haki na ni utambulisho wa kwanza wa mtoto na nyaraka ambayo hutumika kuthibitisha taarifa muhimu za mwananchi kwani inakuwa na taarifa muhimu ikiwemo jina, majina ya wazazi wote wawili, mahali alipozaliwa na tarehe aliyozaliwa hivyo kujua umri wake.
Mkwazu alisema kuwa utekelezaji wa zoezi hilo kitaifa utafanyika kwa muda wa miezi mitatu hivyo ni lazima kuzingatia umakini wakati wa zoezi kwa kuandikisha watoto kwa ufasaha ili mwisho wa siku tuwe na takwimu sahihi za watoto watakaokuwa wamesajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni watakazoelekezwa maana taarifa hizo zitaingizwa kwenye mfumo ambao utatumia simu za mkononi.
Katika hotuba yake, Mkwazu alisema kuwa zoezi la kusajili watoto sasa linakabidhiwa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri na taarifa za watoto zitaanza kuchukuliwa katika ofisi za kata na vituo vya afya na zahanati ambapo maafisa watendaji na watoa huduma watawajibika kuwatafuta watoto walio chini ya miaka mitano ili wapatiwe vyeti vya kuzaliwa bure
Kwa upande wa mwakilishi wa Ofisa usajili kutoka makao makuu (Rita ) mariam gwaja alisema zoezi la kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa linaendelea nchi nzima, elimu inaendelea kutolewa juu ya umuhimu wa kuwa na cheti cha kuzaliwa, wananchi wengi wanaitikia sana hivyo naamini hata masasi zoezi litafanyika kwa mafanikio makubwa.
Kwa kipindi kirefu nchini Tanzania kazi ya utoaji wa cheti cha kuzaliwa imekuwa inafanywa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na udhamini (RITA) ambapo takwimu kwa mujibu wa sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2012 watoto chini ya miaka mitano asilimia 13 tu wamesajiliwa nchi nzima na asilimia 9 kwa mkoa wa Mtwara, hali hii inaonyesha na kuashiria kuwa watoto wengi hawapo ndani ya mfumo.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa