Watendaji wa vijiji na maafisa ugani katika vijiji 97 na kata 30 vinavyotekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika kusimamia mradi huo ili kuwaondolea umasikini wananchi kama adhma ya serikali kwa kuhakikisha kila mlengwa anapata stahiki zake kadri ya muongozo.
Watendaji wa vijiji na maafisa ugani wakifuatilia mafunzo
Maelekezo hayo yametolewa kwa watendaji na maafisa ugani hao katika kikao kazi kilicholenga kuwajengea uelewa juu ya mpango huo kutokana na watendaji wengi wa vijiji kuwa wapya katika utumishi wa umma, hivyo mafunzo hayo yatawapa fursa ya kuelewa wajibu wao katika utekelezaji na usimamizi wa mradi wa kunusuru kaya masikini katika maeneo yao ya kazi kama watendaji wakuu.
mwezeshaji wa mafunzo kwa watendaji na maafisa ugani kuhusu mpango wa kunusuru kaya masikini ndugu Antony Mhando akitoa mada
Akitoa maelekezo hayo kwa watumishi hao katika kikao kazi hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ndugu Jeremiah Lubeleje ameeleza kuwa ili mpango huo ulete manufaa kwa wananchi watendaji ndio wasimamizi wakuu kwa kuhakikisha walengwa wanaostahili wanapata fedha zao kwa mujibu wa miongozo.
Lubeleje amefafanua kuwa, takribani watendaji wa vijiji 80 ni waajiwa wapya ,hivyo kwa ugeni wao hawajui mpango ndio maana tumeamua kutoa mafunzo elekezi juu ya mpango kwa watendaji hawa kwani ndio watendaji wakuu kwenye maeneo yao katika kutekeleza mpango huu wa kunusuru kaya masikini.
washiriki wakifuatilia kwa makini mafunzo juu ya mapango wa kunusuru Kaya masikini
“Ni vema mkafahamu kuwa lengo la serikali ni kuziwezesha kaya masikini kuongeza kipato na kukuza uchumi kupitia ruzuku na vikundi vya kuweka akiba, hivyo ni vema mkasimamia vizuri walengwa ili fedha hizo wazitumie katika matumizi yanayofaa” alisema Lubereje.
Kwa upande wa maafisa ugani, Lubeleje ameeleza kuwa wanapaswa kuhakikisha wanatoa usaidizi wa kitaalamu katika miradi inayoanzishwa na walengwa kupitia vikundi vya kuweka akiba na kukuza uchumi ikiwemo miradi ya kilimo na mifugo kwa kutoa usaidizi juu ya mbinu bora za kulima na kufuga lakini pia namna ya kukabiliana na magonjwa ili wazalishe kwa tija.
Mratibu wa TASAF halmashauri ya wilaya ya masasi Thobias Mkude akisisitiza jambo wakati wa mafunzo kwa watendaji na maafisa ugani kuhusu mpango.
Kuhusu miradi ya ajira ya muda, Lubeleje( kaimu mkurugenzi) amesema watendaji wa vijiji wanapaswa kuelewa kuwa baada ya mradi kukamilika jukumu la kuhakikisha mradi unahudumiwa na kuendelezwa ni la kijiji na sio walengwa pekee, hivyo miradi kama ya upandaji miti inapaswa ihudumiwe na wananchi wote badala ya kuwaachia walengwa peke yao baada ya muda wa utekelezaji wa mradi kuisha.
Kwa upande wake Mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini ndugu Thobias Mkuse amesema kuwa, jumla ya vijiji 97 katika halmashauri ya wilaya ya masasi vinanufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini ambapo jumla ya vikundi 718 vya kuweka akiba na kukuza uchumi vimeundwa ikiwa ni namna ya kuwafanya walengwa wawe na uwezo wa kukuza uchumi hata baada ya mradi kuisha.
mmoja wa washiriki akitoa hoja wakati wa mafunzo
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa