Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara limetoa rai kwa watendaji wa Serikali katika halmashauri hiyo kuepuka kujihusisha na harakati zozote za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, na badala yake watimize wajibu wao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia misingi ya utumishi wa umma.
Wito huo umetolewa katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo Mbuyuni Masasi huku Baraza hilo likieleza wasiwasi wake kuhusu madai ya kuwepo kwa watendaji wanaojihusisha na shughuli za kisiasa, jambo linalotajwa kuwa kinyume na maadili ya kazi za umma na kinachoweza kuathiri utendaji kazi wa Serikali.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Ibrahimu Chiputula amesisitiza kuwa ni marufuku kwa mtumishi yeyote wa umma kushiriki moja kwa moja au kwa namna yoyote katika kampeni za kisiasa, na kwamba Halmashauri haitavumilia vitendo hivyo.
“Tunawahimiza watendaji wetu kubaki kuwa wasimamizi wa sheria na taratibu bila kuegemea upande wowote wa kisiasa. Huu ni wakati wa kuonyesha uaminifu wao kwa wananchi kwa kutimiza majukumu yao kwa haki, uwazi na uwajibikaji,” alisema.
Aidha, waheshimiwa Madiwani wametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa watumishi wote wanakumbushwa wajibu wao na kuchukuliwa hatua stahiki wale watakaobainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Kauli hiyo inakuja wakati Taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, ambapo Maafisa wa Serikali wanatakiwa kutekeleza majukumu yao bila kuathiri mchakato wa kidemokrasia kwa ushabiki wa kisiasa.
14/05/2025
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa