Ili kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya wanawake kwa mwaka 2019 isemayo “Badili fikra, kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu” Wanawake wametakiwa kuwa na mtazamo chanya kufikia maendeleo katika Nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi, kisiasa, kijamii pamoja na kuwa mfano bora kwa malezi ya watoto ili kuwa na jamii yenye maadili mema.
Kauli hiyo ilitolewa na Mgeni rasmi Bi Emmy Rajab Ng’oura ambaye ni Afisa Tarafa wa tarafa ya Lulindi , Halmashauri ya Wilaya ya masasi , katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani , yaliyofanyika jana machi , 8 katika viwanja vya shule ya sekondari Namombwe kata ya Mchaulu.
Mgeni rasmi Bi Emmy Rajab Ng’oura akishiri zoezi la ufyatuaji wa tofali kwa ajili a ujenzi wa Bweni la wasichana katika shule ya sekondari Nambombwe
Akihutubia wananchi wakati wa sherehe hizo, Bi Ng’oura amewataka wanawake wa halmashauri hiyo, kubadili fikra hasi katika kufikia maendeleo, badala yake watumie fursa zinazotolewa na serikali na wadau mbalimbali ikiwemo utoaji wa mikopo isiyo na riba, elimu ya masuala ya usawa wa kijinsia na vitambulisho vya wajasiliamali ili kujikwamua wenyewe katika sekta zote na kutekeleza majukumu yao bila vikwazo vinavyotokana na jinsia.
Bi Ng’oura alieleza kuwa “Moja ya fursa ambayo serikali imeitoa ni kutoa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo kwa bei ya shiringi 20,000 tu, nawasihi wanawake wanaojihusisha na ujasiliamali kuchangamukia fursa hii ili muweze kufanya biashara zenu bila usumbufu wa kutoa tozo zingine zozote”
Aidha alisema kuwa , kumekuwa na matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto, wananwake inawapasa kuwa mstari wa mbele kupinga na kuwafichua watu wanaofanya ukatili wa kijinsia na wale waliofanyiwa ukatili kama ubakaji na ndoa za utotoni, ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na sio kuungana nao kuwaficha wahalifu hao.
Wanawake wakicheza wakati wa sherehe yao
" Ni vema kutambua, wanawake ndio msingi wa mabadiliko kwenye jamii, kama wanawake tutabadili fikra zetu juu ya mambo mbalimbali kuanzia ndani ya familia, jamii zetu pia zitabadika, hakutakuwa na ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto, watoto wote watapata elimu sawa bila kujali jinsia na tutatokomeza ndoa na mimba za utotoni.
Ni jambo la kujivunia kuona Kadri ya siku zinavyoenda wanawake wanashika nyazifa tofauti katika sekta mbalimbali kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, ambapo kwa Halmashauri hiyo jumla ya wananwake 104 wanatumikia nafasi mbalimbali za uongozi “ haya ni mafanikio makubwa tunapaswa kujipongeza” alieleza Bi Ng’oura
Mgeni rasmi Bi Emmy Rajab Ng’oura akimvalisha kitambulisho cha ujasiliamali mmoja ya wanawake katika siku ya maadhimisho ya wanawake duniani
Akisoma taarifa ya utekelezaji mbele ya mgeni rasmi, Afisa Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Neema Joseph amesema kuwa, Halmashauri hiyo imefanya maadhimisho hayo, huku ikiwa na mafanikio makubwa katika kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi, ambapo jumla vikundi 8,vimepatiwa mikopo ya bila riba, yenye thamani ya shilingi milioni 75, fedha zinazotokana na asilimia 10 za mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.
Afisa Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Neema Joseph akisoma taarifa ya utekelezaji
Pamoja na kuadhimisha maadhimisho yaho kihalmashauri katika kata ya mchaulu, afisa maendeleo ya jamii alieleza kuwa sherehe kama hizo pia zinafanywa katika kata zingine kama Mwena, ndanda, chigugu na Nangoo, lengo ikiwa ni kuhasisha wanawake katika maeneo yote kutambua haki na wajibu katika kufikia usawa wa kijinsia ambapo wameshiriki katika shunguli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa miradi, kufanya usafi , kusaidia wagonjwa na kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya "Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu" yamekwenda sambamba na upimaji wa afya kwa magonjwa yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa bure, burudani mbalimbali, mashindano ya mchezo wa mpira wa miguu kwa wananwake na mpira wa pete.
Mgeni rasmi Bi Emmy Rajab Ng’oura akikabidhi vifaa vya shule kwa wanafunzi waishio katika mazingira magumu vilivyotolewa na Chama cha walimu (CWT) na shirika la SWISSAID
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa