Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema jumla ya wapiga kura 26,769,995 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, sawa na asilimia 81.15 ya lengo la kuandikisha watu 32,987,579 ikiwa ni masaa machache kufikia ukomo wa zoezi hilo ifikapo tarehe 20 Oktoba 2024.
Waziri Mchengerwa ametoa tathmini hiyo ya uandikishaji wa wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha kujiandikisha cha Michikichini Kijiji cha Umwe Kaskazini Wilayani Rufiji.
“Mpaka tarehe 19.10.2024 ninaozungumza jumla ya uandikishaji kwa wanaume ni 13,033,988 sawa na asilimia 48.69 na wanawake ni 13,736,007 sawa na asilimia 51.31 ya watu wote waliojiandikisha kuanzia tarehe 11 hadi 19 Oktoba, 2024”, Mhe. Mchengerwa ameeleza.
Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa, mwenendo huo wa uandikishaji ni mzuri na kama utaendelea hivyo ambapo kwa siku ya leo ndio mwisho wa uandikishaji ni wazi kuwa lengo la kuandikisha wapiga kura 32,987,579 litafikiwa.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote waliojitokeza kujiandikisha hadi muda huu ninaotoa tathmini ya uandikishaji, kwani tayari wamejiwekea mazingira kubalika kisheria ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa wanaowataka ifikapo tarehe 27 Oktoba 2024,”Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Akianisha mikoa mitano yenye asilimia kubwa ya uandikishaji hadi kufikia tarehe 18 Oktoba, 2024 ambayo ilikuwa ni siku ya 8 ya uandikishaji, Mhe. Mchengerwa amesema mkoa wa Tanga umefikia asilimia 101.13% ya malengo, mkoa wa Pwani umefikia asilimia 98.74% ya malengo, mkoa wa Mwanza umefikia asilimia 94.09% ya malengo, mkoa wa Dar es Salaam umefikia asilimia 86.66% ya malengo na mkoa wa Dodoma umefikia asilimia 80.63% ya malengo.
Zoezi la uandikishaji wa wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lilizinduliwa Rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan aliyejiandilkisha katika Kitongoji chake cha Sokoine Kijiji cha Chamwino siku ya tarehe 11 Oktoba,2024.
20/10/2024
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa