Walimu wakuu wa shule za msingi 125 wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wapewa mafunzo kuhusu mfumo mpya wa utoaji wa taarifa na takwimu shuleni lengo ikiwa ni kuhakikisha utoaji wa taarifa hizo unakuwa sahihi, rahisi na kwa haraka zaidi.
Mfumo huu unampa nafasi mwalimu mkuu kutuma taarifa na takwimu za shule yake ambazo zitaonekana pia ngazi ya halmashauri, mkoa na OR –TAMISEMI kwa wakati mmoja tofauti na hapo awali ambapo taarifa zilipaswa kutumwa kwa ngazi moja baada ya ningine hali ambayo ilikuwa inachelewa taarifa lakini pia usahihi wa taarifa hizo kuto kuwa kwa uhakika.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Afisa Elimu Ufundi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ndugu Eugeni Ngaeje alisema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI imeamua kuleta mfumo mpya wa utoaji taarifa na takwimu kwenye shule kwa kutumia intaneti ambapo walimu wakuu sasa wataweza kutuma takwimu kila siku bila kupitia utaratibu wa kupeleka ngazi ya halmashauri, mkoani na baadae TAMISEMI.
Ngaeje alisema kuwa walimu wanapata mafunzo kwa vitendo ambapo walimu wote 125 wamepewa vishikwambi (TABLET) kama nyenzo ya kutuma taarifa zao kila siku kwa urahisi zaidi wakiwa shuleni ambapo taarifa hizo zinahusisha maudhurio ya walimu na wanafunzi, taarifa za mapato, vipindi vilivyofundishwa, matumizi ya fedha na taarifa zingine.
Aidha Ngaeje amewaasa walimu kutumia Vishikwambi hivyo kwa malengo kusudiwa na sio kutumia vinginevyo kama kujiunga na mitandao ya kijamii pamoja kufanya kazi kwa bidii kwani utumaji wa taarifa kwa mfumo huu ni wa kila siku.
Pia Ngaeje amewashauri Walimu Wakuu wanashauriwa pia wakirudi katika vituo vyao vya kazi wawafundishe walimu wengine ili hata Mwalimu Mkuu akiondoka au kupata dharura zoezi la utumaji taarifa lisikwame.
Akiongea kwa niaba ya walimu wakuu wengine, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chilolo ndugu Haji Jafari Chipenga alisema kuwa anaishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuanzisha mafunzo hayo ya utoaji wa taarifa na takwimu kwa kutumia njia ya kisasa ambapo walimu wote wamepewa vishikwambi ( TABLET) kwa ajili ya kutuma taarifa kwa haraka na kwa usahihi zaidi kwani zinakuwa zinatoka kwenye chanzo husika.
Pamoja na uboreshaji huo kunauwezekano wa kupata changamoto kwa baadhi ya walimu ambao hawana uzoefu wa matumizi ya vifaa vya Tehama ikiwemo vishikwambi hivyo kwa hatua za mwanzo baadhi ya walimu watashindwa kutuma taarifa kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa