WANANCHI wa Kijiji cha Mbuyuni, Kata ya Mbuyuni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara wametoa jumla ya hekari 200 za mashamba yao bila fidia yoyote ambapo hekari 98 kati ya hizo wametoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Masasi na hekari 102 kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo.
Hayo yalibainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Gelasius Byakanwa jana tarehe 15/01/2019 aliyoifanya kwa ajili ya kuzindua ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya wilaya inayojengwa katika kijiji cha Mbuyuni kata ya Mbuyuni ambapo ujenzi huo tayari umeshaanza kutekelezwa kwa hatua za awali.
Akisoma taarifa ya ujenzi huo wa hospitali ya Halmashauri ya wilaya mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Dkt. Charles G. Mkombe alisema mradi huo wa ujenzi wa hospitali ya wilaya utagharimu jumla ya Shilingi bilioni 7.5 hadi kukamilika na kuwa na jumla ya vyumba 22 vya kutolea huduma.
Dkt.Mkombe alisema serikali imeshatoa jumla ya kiasi cha fedha Shilingi bilioni 1.5 kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza Halmashauri imepokea Shilingi Milioni 500 mwezi Novemba 2018 na mwezi disemba 2018 Halmashauri ilipokea Shilingi bilioni 1.
“Baada ya kupata kibali kutoka Tamisemi cha kuturuhusu kuanza ujenzi na kwamba jengo la kwanza litakuwa la utawala, jengo la pili ni la wagonjwa wa nje, stoo ya dawa, jengo la maabara, jengo la vipimo vya mionzi, na jengo la wadi ya wazazi,” alisema Dkt.Mkombe
Alisema hadi sasa tayari jumla ya fedha Sh.173 milioni zimeshatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ujenzi ambazo zimeshaanza kutekelezwa ikiwemo ununuzi wa mchanga, mawe, kokoto, saruji mifuko, nondo na vifaa vingine mbalimbali, aidha wananchi wameendelea kushiriki ujenzi huo kwa asilimia 100.
Awali akizungumza na wananchi hao kwenye eneo hilo la ujenzi wa hospitali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa aliwapongeza wananchi hao ambao wameamua kujitolea kutoa eneo la hekari 98 ili serikali iweze kujenga hospitali hiyo ya wilaya na kwamba kitendo kilichofanywa na wananchi hao ni cha kizalendo.
Alisema, kitendo cha wananchi kuamua kushiriki ujenzi huo kwa asilimia 100 ni faraja kwake na serikali kwa ujumla. Hivyo serikali itaendelea kuwapatia huduma zote za msingi kwa vile maamuzi yao ni taswira nzuri na kwamba iwapo wananchi wakihamasishwa wanaweza kufanya mambo ya maendeleo bila kushurutishwa.
Wananchi wameipongeza serikali kwa uamuzi wa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga hospitali ya halmashauri ya wilaya, na katika kuiunga mkono serikali yao wameona ni bora wao kama wananchi wajitolee kutoa eneo ambalo awali lilikuwa ni mashamba yao ya kilimo ili serikali iendelee na mchakato wake wa kujenga hospitali hiyo kwani maendeleo ni kwa ajili ya wananchi wote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mhe. Juma Satmah akiwa amebeba tofali alilolifyatua katika uzinduzi wa ujenzi wa hospitali ya Halmashauri, uliofanyika katika kijiji cha Mbuyuni tarehe 15/01/2019.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa