Na EKONI, Edwin Frank
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Seleman Mzee amezindua Baraza la Biashara la Wilaya ya Masasi mwishoni mwa mwezi Mei 2017 lililojumuisha wajumbe kutoka sekta za umma na sekta binafsi na yeye akiwa kama Mwenyekiti wa Baraza hilo kama chombo cha kisheria kusimamia masuala ya biashara wilayani humo.
Akizungumza kwenye kikao cha uzinduzi wa baraza hilo mwenyekiti huyo alieleza kuwa uanzishwaji wa baraza hilo ni wa kisheria kupita waraka wa Rais Na.1 wa mwaka 2001 likiwa na lengo la kuunda jukwaa la majadiliano kati ya Sekta za Umma na Binafsi ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Akiainisha majukumu ya baraza hilo Mkuu wa wilaya alisema kuwa baraza lina wajibu wa kuhamasisha Wafanyabiashara wengi kujiunga na TCCIA ili kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuwa karibu na wafanyabiashara na wakulima ili kujua kero zao na kuwataka walipe kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha Mkuu wa Wilaya alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wajumbe wa baraza hilo kuwa wabunifu kwa kubuni na kuboresha huduma za miundombinu zinazoweza kukaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika maeneo ya wilaya ya Masasi.
Aidha Mkuu wa Wilaya alimelipongeza shirika la Mamlaka ya Maji Masasi Nachingwea (MANAWASA) kwa kutoa huduma bora ya maji kwa wateja wake, aliwasihi kusambaza maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na mradi huo.
Kutokana na Miundombinu ya barabara ya masasi kutokuwa ya uhakika, Mkuu wa Wilaya alisema kuna haja ya baraza hilo kuona namna ya kuboresha miundombinu ya barabara ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Kuhusu suala la umeme amewapongeza wananchi wa Masasi kwa utulivu wao licha ya kero nyingi zilizopo zinazohusiana na umeme, aliliomba shirika la Tanesco tawi la masasi kutumia fursa hiyo kuwasiliana na ngazi za juu ili kuona namana ya kuondoa tatizo la umeme ili kuwavutia wawekezaji kwani kukosekana kwa umeme wa uhakika kunaweza kukimbiza wawekezaji na hata wageni.
Suala la masoko ni eneo linalopaswa kuangaliwa na baraza hilo kwani kuna mazao mengi hayanunuliwi na yanaharibika kutokana na kukosa soko, alisema kuna haja ya kutoa elimu ya biashara kwa wakulima wetu ili waweze kunufaika na kilimo.
Aidha aipongeza shirika la Mapato Tanzania( TRA) Wilaya ya Masasi kwa kasi nzuri ya ukusanyaji wa mapato ambapo alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo Masasi ipo zaidi ya asilimia mia moja (100%) ya ukusanyaji wa mapato na aliwasihi wajumbe wa baraza hilo kuendelea kuhamasisha jamii ili walipe kodi kwa wakati.
Kwa upande wake Katibu wa TCCIA Mkoa wa Mtwara ameeleza majukumu ya baraza la biashara katika ngazi ya mkoa na wilaya ni pamoja na kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara na kuwekeza, kuibua fursa za uwekezaji na kuzindua fursa hizo kwa kupitia makongamano ya uwekezaji pamoja na kuandaa midahalo mahususi.
Katibu huyo alielezea maeneo sita ya uboreshaji wa mazingira ya biashara katika Big Result Now (BNR) kuwa ni pamoja na kuangalia upya mfumo wa kisheria na kitaasisi, upatikanaji wa ardhi na uhakika wa umilikishaji, usimamizi na uratibu wa shughuli za biashara, utitiri wa kodi, tozo na ada, kuzuia na kupambana na rushwa, sheria na stadi za kazi na usimamizi wa mikataba na sheria za kazi.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa