Wazazi na walezi Wilayani Masasi Mkoani Mtwara wametakiwa kuacha tabia au mazoea ya kupeana talaka bila sababu za msingi kwani hiyo ni sasabu kubwa inayopelekea watoto wengi kukosa haki zao za msingi ikiwemo kupata malezi bora, elimu, mavazi na huduma za afya na hivyo kupelekea watoto wengi kukosa fursa sawa kama kauli mbiu ya maadhimishao haya inayosema “Maendeleo Endelevu 2030 Imarisha Ulinzi na Fursa sawa kwa Watoto”
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya masasi Mh. Selemani Mzee wakati akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha mbuyuni Halmashuri ya Wilaya ya Masasi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika Halmashauri hiyo na kuwaeleza kuwa hiyo tabia ni inafanya watoto kukosa haki za msingi huku wazazi wao wakianzisha maisha mengine wakati watoto wanabaki na bibi zao au walezi ambao mara nyingi wanauwa hawana uwezo wa kuwapatia mahitaji ya msingi.
“Tabia ya wanandoa kutalikiana au kwa msemo wa masasi kumwagikana iachwe mara moja watu mkioana na kupata watoto ni vizuri mkabaki pamoja ili mlee watoto lakini pia mnakuwa mfano bora kwa watoto hata wakija kuwa na famila zao watadumu katika ndoa zao” alisema Mzee.
Mhe. Mzee alisema jamii inapaswa kuimarisha ulinzi kwa watoto wote pale inapoonekana kuna dalili za unyanyasaji na kupinga mambo yote yanayohatarisha ustawi na usalama wa watoto wote wawe na furaha wakati wote kwa kuwapenda na kuwajali.
Aidha selemani alitoa rai kwa jamii kupinga na kukemea kwa nguvu zote unyanyasaji wa kijinsia kama kuwanyanyasa watoto kingono, kuwabaka au kuwaingilia kimwili watoto wa kike an unyanyasaji unaweza kuwa wa kihisia mfano kutukana mbele ya watoto au kupigana, kuwatukana, kuwatisha, kuwapuuza, kuwatenga au kuwafanya kichekesho.
Jamii inapaswa kuwapatia elimu watoto kwani hakuna kitu chenye thamani na urithi bora kwa watoto kama elimu, mambo yote wafanye ila elimu liwe ni kipaumbele cha kwanza kwenye kila familia kwa kuhakikisha watoto wanapelekwa kweny program za elimu ya awali, kuwapatia elimu ya msingi na sekondari ambayo kwa sasa Serikali inatoa elimu hii bure lakini pia ni muhimu watoto wanaomaliza darasa la saba kuwapeleka kwenye shule za ufundi stadi.
Pia wazazi/walezi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuhakikisha mazingira wanayoishi watoto yanakuwa safi na salama kuanzia wao wenyewe hadi mavazi yao na kuwa wepesi kuwapeleka watoto wao hospitali pindi tu wanapougua lakini wasisite kuwapeleka watoto kupata chanjo za magonjwa kama kifua kiuu, polio, kifaduro, donda koo homa ya ini, tetenasi nk. Kwani chanjo hizo huzuia watoto wasiambukizwe na magonjwa hayo.
Amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuwaajiri na kuwafanyisha kazi ngumu watoto lakini amewaomba kuungana kwa pamoja kuwaepesha watoto na kazi zote hatarishi na badala yake watoto waweze kusaidia kazi ndogondogo na si vinginevyo.
Bibi Changwa Mkwazu, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Masasi akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa Wilaya, alisema kwa mwaka 2016/2017 halmashauri ya wilaya ya masasi imeendelea kuwasaidia watoto walio katika mazingira hatarishi ambapo katika bajeti yake imetenga Tsh. 7,984,000 kwa ajili ya kuwasaidia kupata huduma muhimu za shule kama vile kalamu, daftari na sare.
Pia halmashauri ya wilaya ya masasi kupitia Idara ya afya imefanikiwa kuwapatia sare za shule, kalamu watoto wapatao 150 zenye thamani ya Tsh. 2,250,000 na kuwakatia kadi za Bima ya afya ya Jamii (CHF) zenye thamani ya Tsh. 250,000 kwa lengo la kuwawezesha watoto hao kupata huduma za msingi.
Halmashauri ya wilaya ya masasi imefanikiwa kutoa chanjo ya Vitamini A kwa watoto 3742 walio chini ya miaka mitano kati ya watoto 2449 waliotarajiwa, pia imetoa chanjo ya kuzuia Kifua Kikuu kwa watoto 3548 kati ya watoto 2449 waliotarajiwa sawa na asilimia 144.
Pia halmashauri imetoa chanjo ya Polio kwa watoto 3361 kati ya watoto 2449 waliotarajiwa, chanjo ya kuzuia kifaduro, dond koo, homa ya ini na tetenasi kwa watototo 3396 kati ya watoto 2449 tarajiwa sawa na asilimia 138
Bi Changwa alisema kupitia kitengo cha Ustawi wa Jamii, halmashauri imefanikiwa kushughulikia matatizo mbalimbali ya ya watoto yahusuyo ukatili na unyanyasaji wa watoto ambapo imefanikiwa kutatua na kutoa ushauri wa kisaikolojia kwa watoto wapatao thelathini na mbili na kutoa msaada wa kisheria kwa watoto kumi na moja.
Kwa naiaba ya halmashauri ya wilaya ya masasi yaliyashukuru mashirika yasiyo ya kiserikali (NG’OS na CBO’S), waheshimiwa madiwani, viongozi wa kata na wadau wengine waliowezesha halmashauri ya wilaya ya masasi kufikia mafanikio hayo nab ado anawaomba kuendeleza ushirikiano ili kuwafanya watoto kupata ulinzi na furaha sawa na hatimaye Tanzania ipate maendeleo endelevu.
Siku ya mtoto wa afrika duniani huadhimishwa na kukumbuka mauaji ya watoto zaidi ya mia sita (600) yaliyotokea huko nchini afrika ya kusini kwenye kitongoji cha soweto mwaka 1976”, mhe. selemani mzee, mkuu wa wilaya ya masasi alisema.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa