Baada ya uchunguzi kufanyika juu ya vurugu zilizofanywa na wanafunzi wa shule ya sekondari chidya tarehe 1 septemba 2018 na kusababisha hasara ya zaidi ya milioni 18, Bodi ya shule ya sekondari chidya imefikia maamuzi ya kufukuza wanafunzi 23 huku wanafunzi 8 wakisimamishwa shule kwa muda wa siku 21.
Maamuzi hayo yametolewa tarehe 27 septemba, 2018 baada ya kupitia taarifa za uchunguzi wa tukio hilo na kujiridhisha pasipo na shaka yoyote kuwa wanafunzi hao wanastahili adhabu hiyo kwani wamekutwa na hatia. Aidha taarifa ya bodi imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kukomesha tabia za migomo shuleni hapo na kutoa fundisho kwa wanafunzi waliobaki.
Afisa elimu sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya shule ya sekondari ya Chidya ndugu Juma Kasandiko, ameeleza kuwa sababu kuu zilizofanya wanafunzi 23 waliofukuzwa shule ni majina yao kutajwa na vyombo zaidi ya vitatu vya uchunguzi, kutoka nje ya shule baada ya kufanya vulugu na kutorejea jambo ambalo ni kinyume na sheria za shule.
Kasandiko amefafanua kuwa wanafunzi 23 waliofukuzwa shule kati yao 6 ni kidato cha sita, 12 ni kadato cha nne na 5 kidato cha tatu.
Kwa wanafunzi wa kidato cha nne ambao wamefukuzwa shule, bodi imewapa fursa ya kurudi kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya kidato cha nne kwasababu wameshasajiliwa kufanya mtihani huo.
Kuhusu fidia ya hasara iliyosababishwa na vurugu hizo, ndugu Kasandiko ameeleza kuwa italipwa na wananfunzi wote walioshiriki mgomo yaani wanafunzi 23 waliofukuzwa shule, wanafunzi 8 waliosimamishwa shule kwa siku 21 na wanafunzi 251 walioshiriki kwenye vurugu lakini hawakuondoka shuleni baada ya vulugu na hawakutajwa mara nyingi kwenye ripoti za uchunguzi kama vinara wa vurugu hizo ambapo kila mwanafunzi atatakiwa kulipa shilingi 64,000.
“Hatua hizi za kinidhamu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Chidya waliofanya vurugu na kusabaisha hasara na utulivu wa shule, ni fundisho kwa wanafunzi wanaobaki na shule zingine zote kwani sheria zitaendelea kuchukuliwa kwa wanafunzi wote wanafanya vurugu shuleni ikiwemo kufukuzwa shule” alisistiza Kasandiko.
Aidha ndugu Kasandiko amewasistiza walimu kuwa “ni vizuri mkasimamia sheria za shule kwa kujiwekea utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wanafunzi ili kubaini haraka matatizo ya wanafunzi na kuyatatua, pia kwa walimu wanaoshirikiana na wanafunzi kuhamasisha migomo tabia hiyo muache kabisa kwani sitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu. Mfanye kazi kwa kuzingatia sheria na miongozo ikiwemo kuwa walezi na sio kuhamasisha wanafunzi kufanya vurugu”
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo mwalimu Zawadi Mdimbe amezishukuru kamati za uchunguzi kwa kufanya kazi zao vizuri ambapo taarifa zilizowasilishwa zimeiwezesha bodi ya shule kutoa maamuzi bila upendeleo au kumwonea mtu yeyote na hatimaye sasa shule itakuwa na utulivu na amani na kuendelea kutekeleza majukumu ya kila siku ikiwemo maandalizi ya mitihani ya kitaifa.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa