Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais,Ikulu (kazi maalumu) mhe.George Huruma Mkuchika amewataka Wakulima wa Mkoa wa Mtwara na Lindi kuhakikisha mafunzo waliyopata kwenye maonyesho ya nane nane yakawe chachu kwa kuongeza uzalishaji Katika mazao ya kilimo, mifugo pamoja na uvuvi.
Mkuchika ametoa agizo hilo jana tarehe 08/08/2024 katika kilele Cha maadhimisho ya siku ya Wakulima, Wafugaji na wavuvi (nane nane) kanda ya kusini yanayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo yamefanyika katika viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inadhamira ya dhati ya kuhakikisha inawainua Wakulima, Wafugaji na wavuvi ili wazalishe kwa tija sambamba na uimarishaji huduma za ugani, Kutoa ruzuku kwenye pembejeo na kuweka mifumo safi ya masoko ya bidhaa za kilimo.
Amesema maonyesho hayo ya mwaka huu ambayo yamefana sana na wananchi wamepata nafasi kubwa ya kujifunza mengi kutoka kwa Wataalamu na wadau mbalimbali anaomba sasa yakawe chachu kwao na wengine katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara yakiwemo mihogo, mahindi, mtama na Mazao jamii ya mikunde, " Wananchi wa Mtwara na Lindi wataishi vizuri kwenye kaya zao kama Nyumba zao zitajitosheleza kwa chakula, mkuu wa Wilaya naye ataishi kwa furaha anapoona Wilaya yake
inajitosheleza kwa chakula na Mkoa pia utakuwa unajitosheleza kwa chakula."
Mhe.Mkuchika ameongeza kuwa wamekuja hapo Katika maonyesho hayo sio kufanya sherehe bali kuboresha kilimo chao, kuboresha uvuvi wao pamoja na ufugaji kwasababu Leo hii katika dunia nzima suala linalopigwa vita ni kupambana na umaskini hivyo waendelee kuwatumia wataalamu wa kilimo waliopo katika Kata zao waelekezwe Namna bora ya kufanya na kuongeza uzalishaji ili kuweza kupambana na umaskini.
Aidha amehitimisha kwa Kutoa shukrani kwa mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa kuwapatia Wakulima wa korosho pembejeo za bure hivyo amewahimiza Wakulima kuunga mkono jitihada hizo kwa kuongeza jitihada katika kutunza mashamba ili kuongeza uzalishaji kwakuwa Serikali imedhamiria kuliongezea thamani zao hilo kwakuacha kuuza korosho ghafi.
Maonyesho hayo ya 31 ya nane nane Kanda ya kusini yamefungwa rasmi na mhe.George Mkuchika ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (kazi maalumu) yameenda sanjari na zoezi la utoaji zawadi kwa waliofanya vizuri katika maonyesho ya bidhaa mbalimbali za kilimo, Uvuvi na Mifugo ambapo Halmashauri ya Wilaya Masasi imeendelea kushika nafasi ya pili huku ikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Hata hivyo ifahamike kuwa maonyesho hayo kitaifa yamefanyika jijini Dodoma huku yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, "Chagua Viongozi Bora wa Serikali za MITAA kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi"
09/08/2024
@... Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa