Chama kikuu Cha Ushirika MAMCU LTD mapema June 14, 2024 kimefanikiwa kuingiza mnadani na kuuza jumla ya kilo 13,140,644 za zao la Ufuta, kwa bei ya juu shilingi 3410 na bei ya chini ikiwa ni 3303 huku kilo 4,189,725 zikikosa soko.
Mnada huo ambao ni wa Kwanza umefanyikia katika viunga vya Shule ya Sekondari ya Chiungutwa iliyopo katika Kata ya Chiungutwa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara na Viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya, wakulima, na wafanyabiasha wakishiriki huku mfumo mpya wa soko la bidhaa yaani TMX ukitumika.
Akizungumza mbele ya Wakulima hao Mwenyekiti wa Chama kikuu Cha Ushirika MAMCU LTD Bw.Azam Jurajura amesema "tumefanya mnada wa Kwanza katika chama chetu Cha MAMCU, na kilo ambazo ziliingia ni milioni 13,140,644, na kilo ambazo zimeuzwa ni kilo (milioni nane, laki tisa hamsini na tisa elfu miamoja kumi na tisa) na zilizobakia ni kilo milioni 4,189,725 ambazo hizi sasa zitaingia sokoni katika mnada ujao ambao utafanyika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, kwaiyo niwaombe Wakulima muwe na subira kwasababu makusanyo ambayo tumekusanya Safari hii hatukutarajia kama ufuta unaweza ukawa mwingi kiasi hiki, hivyo niendelee kuwaomba Wakulima sasa tujianadae Kutoa mizigo yetu kwa haraka kwasababu Ufuta bado unaendelea kushushwa ni vyema mkawaisha maghalani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe.Lauteri John Kanoni akitoa salamu za Wilaya mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo amesema zoezi hilo linalofanyika ni la kisasa na ni maelekezo ya Serikali kuingia kwenye mfumo huo wa kidigitali ambao unafanyika wa uwazi na kila mtu anaona kinachofanyika, hivyo anaipongeza Serikali kwa kuwaletea mfumo huo ambao ni mzuri na wataendelea kuutumia.
Wakati huo huo mhe.Kanoni amehitimisha kwa Kutoa tahadhari kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa Kipindu pindu ambao umegundulika katika Kijiji Cha Miesi kata ya Lupaso."tuchukue tahadhari tuzingatie usafi"
Nao kwa upande wao Wakulima ambao wameshiriki katika mnada huo pamoja na kuipongeza Serikali kwa kuwaletea mfumo mpya wa TMX ambao umekuwa ni wa uwazi na manufaa kwao Lakini pia wameishukuru Serikali kwa kuwasimamia na kuhakikisha wanauza Ufuta kwa bei nzuri ambayo inawapa faraja kuendelea kulilima zao hilo.
Imeandaliwa na Winifrida Ndunguru
Afisa Habari MDC
Kazi iendeleeee!
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa