Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ndanda na Lulindi Ndg. Keneth Mgina amewataka Makarani waongozaji wa vituo vya kupigia kura uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa makarani waongozaji wa wapiga kura yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi-Mjini, amewataka
makarani wote kutumia vyema nafasi waliyopewa kwa uaminifu na weledi mkubwa.

“Ninyi mliopo hapa leo mmeteuliwa kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 74 kifungu cha sita cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na tangu tarehe ya uteuzi wenu mnao wajibu wa kikatiba wa kutekeleza majukumu ya uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bara na Madiwani kwa niaba ya Tume katika vituo vya kupigia kura mlivyopangiwa, hivyo yawapasa mtambue kuwa mnategemewa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya INEC mtakayopewa hadi kukamilika kwa zoezi la uchaguzi,” alisema Mgina

Aidha, aliwakumbusha makarani hao kutunza siri za taarifa na vifaa vya uchaguzi, pamoja na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha migogoro au kuathiri amani katika vituo vya kupigia kura.

Amesisitiza kuwa makarani ni kiungo muhimu kati ya wananchi na Tume ya Uchaguzi, hivyo wanapaswa kuwa mfano wa uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yamehusisha makarani wa vituo 623 vya kupigia kura vilivyopo katika kata 34 za Jimbo la Ndanda na Lulindi ambapo washiriki wamefundishwa kuhusu wajibu na majukumu ya makarani waongozaji wa wapiga kura, pamoja na namna ya kuwapokea na kuwaongoza wapiga kura katika vituo vya kupigia kura kwa kuzingatia kanuni za huduma kwa wateja.

Mgina alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka makarani hao kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo, akisisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka huu unahitaji uadilifu, umakini na uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwa watendaji wote wa Tume.
25/10/2025
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa