Maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata Leo tarehe 05/10/2024 wamepatiwa mafunzo kuhusu usimamizi na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa zamani wa Halmashauri hiyo uliopo Masasi mjini yamehusisha Maafisa maendeleo ya jamii kutoka kata zote 34 za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi huku lengo kubwa likiwa ni kuimarisha uelewa kuhusu mikakati ya usimamizi wa maendeleo ya jamii, hususani katika kusimamia mikopo ya asimia 10 kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa.
Aidha wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Maafisa maendeleo ya Jamii ngazi ya Halmashauri hiyo wakiongozwa na Bw. Rashid Njozi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, ambapo amesisitiza umuhimu wa mikopo hiyo katika kuboresha maisha ya wanajamii, na kuwataka maafisa hao kuyazingatia mafunzo ili kuboresha zaidi utendaji kazi wao katika kusimamia mikopo hiyo.
“Mikopo hii inatoa fursa kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu kujiendeleza kiuchumi na hivyo kuchangia katika maendeleo ya jamii nzima, ni matumaini yangu kwamba mafunzo haya mtaongeza mara dufu utendaji wenu na pia yatasaidia kuleta mabadiliko chanya.” amesema Njozi
Mbali na hayo, katika kipindi cha mafunzo, washiriki wamehusishwa moja kwa moja katika mijadala, ambapo wameweza kutoa mawazo na maswali kuhusu usimamizi wa mikopo hiyo, pia mafunzo hayo yametoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kukuza mbinu bora za kazi.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Masasi Bi. Beatrice Mwinuka amewaasa washiriki wa mafunzo kuhakiksha wanakwenda kuhamasisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuunda vikundi Ili waweze kunufaika na fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Mwinuka amesema kuwa halmashauri itaendelea kutoa mikopo kwa walenga lengo kuona makundi hayo yananifaika kiuchumi.
" Kwa mafunzo hayo mliopata hapa leo naomba nendeni mkawe mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa fursa ya mikopo hii ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwani serikali inatoa fedha nyingi kupitia fursa hii,"...alisema Mwinuka.
Hata hivyo maafisa hao wa maendeleo ngazi ya kata pamoja na mambo mengine wamepata nafasi ya kujifunza taratibu za kuandika maombi ya mikopo pamoja na namna ya kusimamia fedha hizo kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa .
Katika hatua nyingine maafisa hao pia wamekula kiapo cha uadilifu katika kusimamia kile wanachokwenda kukitekeleza juu ya usimamizi na uhamasishaji wa mikopo ya asilimia 10 kwenye maeneo na mwisho wamehimizwa kuendeleza elimu waliyoipata kwa vikundi vyao ili kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo na kusaidia katika kuboresha maisha ya jamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Masasi inaamini kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya mabadiliko chanya katika maendeleo ya jamii, kwasababu yana umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano Kati ya Halmashauri na vikundi vya Maendeleo.
@.. Masasi DC
05/10/2024
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa