Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Masasi wamefanya maandamano ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia rasilimali za taifa ikiwemo suala la kuzua usafirishaji wa mchanga wa madini maarufu kama Makinikia leo tarehe 22.06.2017 katika viwanja vya ofisi za Mkuu wa wilaya ya masasi.
Akisoma risala ya Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Masasi, mwenyekiti wa vijana wa chama hicho ndugu Ahmed Matipula alisema kuwa Vijana wa CCM wanapata faraja kubwa kwa kazi mbalimbali zinazofanywa na mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dr. John Pombe Magufuli kwamba Chama cha Mapinduzi kinaendelea kupata heshima kubwa kitaifa na kimataifa kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za kuomba ridhaa ya kuongoza nchi.
Matipula alisema kuwa maandamano hayo ni matokeo ya kazi kubwa anayofanya Rais katika kuwaletea maendeleo watanzania na kumfanya kila mtanzania aishi kwa haki na usawa kwani katika kipindi kifupi cha utawala wake mengi yamefanyika mambo mengi ambayo yanawafanya Jumuiya ya Vijana CCM kutembee kifua mbele hususan pale alipodhibiti matumizi yasiyo ya lazima na nidhamu ya matumizi katika fedha za umma.
Rais ameonyesha ujasiri na uzalendo wa hali ya juu katika dhamira yake ya kudhibiti raslimali za taifa ambazo zilikuwa zinaporwa kiholela hasa madini, alizuia usafirishaji wa makontena yenye mchanga wenye madini (Makinikia) na kuunda tume mbalimbali mfululizo kuchunguza uhalisia wa madini yaliyo kwenye mchanga huo lengo ikiwa ni kujiridhisha kiasi cha madini ambacho kimekuwa kikipotea kwa miaka mingi, alisema Matipula.
Kutokana na jitihada hizo za Mhe. Rais, anapaswa kupongezwa kuliko kubezwa, anahitaji kuungwa mkono na kila mtanzania mzalendo na mpenda maendeleo kwani kiasi kilichopatikana kwenye madini pekeyake kinaweza kuiwezesha bajeti ya mwaka mzima bila kutegemea wahisani.
“Fedha hizo zitasaidia kupunguza vifo vya akinamama na watoto kwa kuwa na huduma bora za afya ya uzazi, zitanunua madawa na pembejeo za kilimo, zitalipa ada za wanafunzi, zitajenga shule, zahanati na vituo vya afya na hospitali. Kwa ujumla fedha hizo zitainua kipato cha Mtanzania na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati”. Matipula alisema.
Bwana Matipula alisema kuwa Jumuiya ya Umoja wa Vijana Wilaya ya Masasi inaunga mkono juhudi za Rais na Serikali yake kwa kuitendea haki Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kiwango kikubwa na kwa vitendo. Aidha anawaomba watendaji wote wa serikali na wadau wengine wa maendeleo kumuunga mkono Rais kila mmoja na eneo lake la kiutendaji.
Matipila anamuomba Rais awapuuze wale wote wenye nia ya kumrudisha nyuma katika jitihada zake za kuwatumikia watanzania na ikibidi kuwashughulikia wale wote watakaobainika wanakula njama wa wawekezaji kwa nia ya kuhujumu juhudi zake za kulinda raslimali za taifa kwa niaba ya watanzania wote.
Aidha jumuiya hiyo imeomba Rais awashughulikie wale wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine kuiingiza nchi yetu kwenye mikataba ya kinyonyaji ambayo inaipa hasara Tanzania kama ambavyo tumeona wale ambao walihusishwa na sakata la ESCROW walichukuliwa hatua.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa