Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Mhe. Selemani Mzee amewataka waratibu elimu kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kufanya kazi ya ufuatiliaji na usimamizi wa taaluma na miundombinu ya shule katika maeneo yao, ili kuboresha elimu ikiwemo kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari kutokana na kuwa na usafiri wa uhakika.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi mhe Selemani Mzee akijiandaa kuendesha pikipiki kabla ya kukabidhi kwa waratibu elimu kata
Mkuu wa wilaya ametoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pikipiki 34 kwa waratibu elimu kata wa Halmashauri hiyo lengo ikiwa ni kuwawezesha waratibu hao kuwa na usafiri wa uhakika kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kufuatilia na kusimamia masuala ya elimu ili kuboresha sekta ya elimu katika shule zote zilizopo katika kata 34 maana hakuna kisingizo cha kushindwa kuzifikia.
“Kuanzia sasa ubora wa elimu utaongezeka kwani Waratibu elimu kata mtakuwa na uwezo wa kupita katika shule zote kuangalia mahudhurio, ufundishaji na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa katika shule hizo za msingi na sekondari kwa fedha za Serikali au nguvu za wananchi” alieleza Selemani
Mkuu wa Wilaya ya Masasi mhe Selemani Mzee akiendesha pikipiki kabla ya kukabidhi kwa waratibu elimu kata
Aidha Mkuu wa Wilaya amewakumbusha Waratibu elimu kata kuwa pikipiki walizokabidhiwa ni kwa ajili ya kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na masuala mengine ya elimu, hivyo pikipiki hizo zikafanye kazi iliyokusudiwa ya kusimamia elimu na sio kutumia kwenye shughuli zenye maslahi yao binasfi ikiwemo kwenda nazo mashambani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mhe. Juma Satmah ameiishukuru Serikali kwa kutoa pikipiki kwa waratibu elimu kata 34 kwani zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza usimamizi wa utoaji wa elimu katika shule za Msingi na Sekondari na hatimaye ufaulu kuongezeka kwani kutakuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara tofauti na hapo awali ambapo waratibu hawakuwa na usafiri wa uhakika kuzifikia shule katika maeneo yao.
Mratibu elimu kata wa kata ya Mbuyuni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi akiendesha pikipiki Baada ya kukabidhiwa leo tarehe 13.07.2018 katika hafla ya kukabidhi pikipiki hizo kwa waratibu elimu kata 34 nje ya Ofisi za Halmashauri.
Satmah amewakumbusha waratibu kuzituma vizuri pikipiki hizo kwani hivyo ni vyombo vya moyo hivyo lazima wazingatie taratibu za kuviendesha vyombo hivyo ikiwemo kuwa na leseni.
Akisomba taarifa ya mapokezi ya pikipiki hizo 34 za waratibu elimu kata zilizotolewa na serikali kuu Afisa elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Elizabeth Mlaponi alieleza kuwa changamoto kubwa inayosababisha kukosekana kwa utekelezaji wa mkakati wa ufuatiliaji na usimamizi wa taaluma na miundombinu shuleni in pamoja na ukosefu wa usafiri, hivyo pikipiki hizo zitarahisisha shughuli za ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za maendeleo ya elimu kwani wataweza kutebelea shule wakati wote na hivyo kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji unafanyika kadri ya mipango ambayo ndio njia mojawapo ya kuongeza ufaulu.
Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Elizabeth Mlaponi Akisoma taarifa ya mapokezi ya pikipiki 34 za waratibu elimu kata
Akiongea kwa niaba ya waratibu wengine baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo Lulu Millanzi alisema kuwa pikipiki hizo zitawasaidia sana kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi tofauti na hapo awali ambapo mazingira ya utendaji kazi yalikuwa magumu sana hali ambayo hata utekelezaji haukuwa wenye ufanisi mkubwa.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutukumbuka na tunaahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kuhakikisha tunafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara shuleni lengo ikiwa ni kusimamia masuala ya elimu na hatimaye kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika shule zetu za msingi na sekondari” alisema lulu.
Pikipiki hizo walizopatiwa waratibu hao ni miongoni mwa pikipiki zilizotolewa na serikali kwa waratibu elimu wa Kata wote hapa nchini zenye lengo la kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa waratibu hao.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa