Walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi wamenufaika na mradi huo baada ya kushiriki utekelezaji wa miradi ya ajira za muda (PWP) na kisha kulipwa ujira katika miradi iliyoibuliwa na kutekelezwa kwenye maeneo yao yenye thamani ya shilingi bilioni 1,346,672,000.
Wananchi wa kijiji cha chiwata wakichota maji katika kisima kilichochimbwa kupitia Mradi TASAF
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo katika vijiji 97 vinavyotekeleza miradi ya ajira ya muda , Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri hiyo Thobias Mkude alisema kuwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, jumla ya shilingi milioni 934,082,900 zilitumika kulipa ujira kwa walengwa walioshiriki kufanya kazi huku milioni 412,589,100 zikitumika kununua vifaa na kugharamia mafunzo na posho za wasimamizi wa miradi hiyo.
Mkude alifafanua kuwa, miradi iliyotekelezwa ni pamoja na miradi ya maji iliyohusisha uchimbaji wa visima 30, mabwawa 4, kusambaza maji ya bomba 1 na miradi ya upandaji wa miti 62 ambapo walengwa walifanya kazi katika miradi hiyo kwa muda wa siku 60 na kulipwa ujira wa shilingi 2300 kwa siku lengo ikiwa ni kuziongezea kipato kaya hizo masikini.
Mradi wa upandaji miti uliotekelezwa kupitia mradi wa TASAF kijiji cha Namajani
Mkude ameeleza kuwa jumla ya kaya 10,559 zinanufaika na mpango huo wa kunusuru kaya masikini kupitia mradi wa Ajira ya muda (PWP), aidha kaya hizo pamoja na kupata ujira huo lakini pia zinaendelea kupata ruzuku ya kila mwezi lengo likiwa ni kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi ikiwemo chakula, kuboresha makazi, kupata huduma za afya na elimu pamoja na kupata mtaji wa kufanya biashara.
Bibi Amina rashidi Musa ambaye ni mmoja wa walengwa wanaonufaika na mpango katika kijiji cha Namajani katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi alisema, anaishukuru serikali kwa kuleta mpango wa TASAF kusaidia kaya masikini kwa kuwapa ujira baada ya kufanya kazi kwenye miradi ya ajira ya muda ambayo kwa sasa inafaidisha jamii nzima na si walengwa pekee
Amina alieleza kuwa, kwa sasa walengwa wengi wameboresha maisha yao kwani wanauhakika wa kupata chakula, kujenga makazi bora , kupata pembejeo za kilimo, kuwa na mtaji wa kufanya biashara pamoja na kukuza uchumi wetu kupitia vikundi vyao vya kuweka akiba jambo ambalo kabla ya mradi hawakuwa na uwezo huo
Bi Neema Luka Ismail akiwa Mlengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika kijiji cha Namajani akiwa amesimama katika nyumba yake aliyojenga kuitia mradi wa TASAF
“Kupitia maradi huu ninakula vizuri ninalala vizuri lakini pia nimeweza kununua bati 20 na kufyatulisha tofali, lakini pia nimeweza kununua dawa za kupulizia mikorosho yangu ili kuongeza uzalishaji , hivyo naishukuru sana serikali kwa mpango huu maana unanisaidia sana” alibainisha Amina
Bibi amina aliongeza kuwa kutokana na fedha anazopata ameweza kujiunga na bima ya afya jamii (CHF) inayomwezesha kupata huduma za afya kwa mwaka mzima yeye na familia yake pamoja na kumununulia mahitaji ya shule mjukuu wake.
Kwa upande wake Fidelis Wiliamu Mmavele mlengwa wa mpango katika kijiji cha Namnajani, alikiri kuwa utekelezaji wa mradi wa kupanda miti katika kijiji chao pamoja na kuwezeha walengwa kuongeza kipato lakini mradi huu umesaidia jamii kupata ujuzi wa namna ya kupanda miti na umuhimu wake baada ya miti hiyo kukua vizuri na kufanya mazingira kuwa mazuri.
Wananchi wa kijiji cha chidya wakichota maji katika kisima kilichochimbwa kupitia Mradi TASAF
“Miti hii inafanya mazingira kuwa mazuri lakini pia shamba hili la miti litaongeza chachu kwa wananchi kupanda miti katika maeneo yao kwa matumizi mbalimbali katika jamii kibiashara na kijamii ikiwemo utengenezaji wa madawati na ujenzi wa miradi ”
Baada ya kukamilika kwa Mirad yote ya ajira ya Muda iliyotekelezwa katika vijiji 97 jukumu la usimamizi wa miradi hiyo unafanya na serikali za vijiji na sio walengwa kwani miradi hiyo kwa sasa ni mali ya kijiji.
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa