HALMASHAURI YA WILAYA YA MASASI YAPATA HATI SAFI .
Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara imepata hati safi kwa miaka mitano (5) mfululizo huku Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akiipongeza Halmashauri hiyo na kusema kuwa imetimiza kwa vitendo agizo la Serikali Kwa asilimia 100%.
Hati hiyo safi ni muendelezo wa upatikanaji wa Miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2018/2019.
Hayo yameelezwa Leo julai 02/2024 Katika kikao maalumu Cha Baraza la Madiwani Cha kujadili na kupitia hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023 kilichofanyika Katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo Mbuyuni Masasi.
Akizungumza katika baraza hilo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Kenani Sawala, Mkuu wa Wilaya ya Masasi mhe.Lauteri John Kanoni amesema "Mkuu wa Mkoa wa Mtwara anawapongeza sana Kwa kupata hati safi kwa muda wa miaka mitano mfululizo, pili anampongeza mwenyekiti na Kamati yake, Pamoja na Watendaji kwa kujibu hoja nyingi ambazo zimetoka kwenye hoja 18 na kubakiwa na hoja 4 ni umahiri mkubwa hivyo anaamini kwa mwaka ujao hoja zote zitamalizika, hongereni sana".
"Pia nawapongeza waheshimiwa Madiwani kwasababu nyie ndio mnaotoa maamuzi ya kuhakikisha mnatekeleza kwa vitendo yale maelekezo ya Serikali yakupeleka fedha kutokana na mapato ya ndani ili ziende kwenye Shughuli za maendeleo kwaiyo mmewatendea vyema wapiga kura wenu.
Aidha mhe.kanoni Katika kuhitimisha taarifa yake ametumia nafasi hiyo Kutoa maelekezo kwa Halmashauri kuwa, "katika mwaka huu mpya wa fedha ulioanza, Mkuu wa Mkoa hapendi kuona katika mkoa wa Mtwara mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan analeta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo na hatmaye kushindwa kutumia fedha hizo kwa wakati alafu zinarudi tena Serikalini lazima tutambue kuwa hatuwatendei haki Wananchi, hivyo kuanzia mwaka huu wa fedha ulioanza mjipange fedha zote mnazozipata zitumike ipasavyo na kuhakikisha zinamalizika.
Beatrice Mwinuka ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, awali akiwasilisha taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023 amesema Katika kutekeleza jukumu lake la kisheria chini ya ibara 143 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kifungu cha 10, kifungu kidogo cha kwanza, na Sheria ya ukaguzi wa umma kifungu namba 148, Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali Kwa mwaka wa fedha ulioishia june 30, alikagua Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na Kutoa maoni yake huru.
Amesema katika utoaji wa maoni ya Mdhibiti na Mkaguzi kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30/06/2023 alikagua mahesabu ya Halmashauri na kupitia majibu ya hoja kutoka timu ya Menejimenti na hatmaye Kutoa hati safi.
Mwinuka ameongeza kuwa, utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali Kwa mwaka 2022/2023 kwa Mwaka huo Ofisi ya CAG ilitoa mapendekezo 18, ambapo hoja 14 zimefanyiwa kazi na kufungwa na hoja 4 zipo kwenye utekelezaji, na pia kulikuwa na maagizo nane (8) kutoka Kamati ya bunge, 6 yamejibiwa na mawili yapo kwenye utekelezaji.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Ndg.Ibrahimu Chiputula amesema Halmashauri hiyo imeendelea kufanya vizuri na kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo ni kutokana na kazi kubwa ambayo wanaifanya wao na Watendaji kwa Umoja (team) hivyo anawashukuru na kuwapongeza sana,
"pongezi hizi ambazo zitatolewa kwa kupata hati safi ni kazi kubwa tunayoifanya sisi na Watendaji wetu, hivyo niendelee kuwaomba Wataalamu tunapoletewa fedha za miradi tuhakikishe hazirudi hazina bali zinatumike zote kwani katika Maeneo yetu bado Kuna miradi mingi ambayo inahitaji kutekelezwa.
Imeandaliwa na:
Winifrida Ndunguru -Afisa Habari Masasi DC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa