Na:Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini (H/W) Masasi.
Nyumba ni Choo! Huu ni usemi ambao hutumika mara nyingi ukiangazia umuhimu wa choo bora na huduma za kujiweka safi nyumbani.
Choo kinaweza kuwa sehemu ya kawaida mathalani shimo refu katika ardhi, lakini kutokana na mahitaji ya faragha ni muhimu choo kuwa na kijumba na mlango.Banda au kijumba kinaweza kutengenezwa kutokana na vifaa vya kawaida, au kutokana na mchanga au saruji.
Usafi katika jamii ni muhimu sana kama ulivyo
kwa mtu binafsi na familia, usafi wa Mazingira humainisha usafi wa jamii kutumia vyoo safi na salama, kulinda usafi salama wa vyanzo vya maji na utupaji salama wa taka, huku suala la uchafuzi wa Mazingira inaelezwa husababisha magonjwa na vifo vingi ambavyo vingeweza kuepukika.
Juhudi yeyote ile ya jamii kwa ajili ya kuboresha usafi wa Mazingira lazima iwasidie watu kuondokana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kawaida.
Na ndio maana kwa kulitambua hilo, timu ya Wataalamu kutoka Idara ya Afya kwa kushirikiana na Kitengo cha Udhibiti wa taka na usafi wa Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mapema tarehe 26 Septemba 2025 ikiwa ni siku ya Afya Mazingira duniani, ilifanya mkutano na wananchi wa Kijiji cha Mbuyuni huku lengo kubwa likiwa ni kuwapa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayoendana na uchafuzi pamoja na usafi wa Mazingira.
Bw.Said Ame ni Afisa Afya Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Masasi akizungumza katika mkutano huo amesema jamii inatakiwa ihakikishe inajenga na kutumia vyoo bora ili kuepuka kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko na kujenga tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na kuendelea kuimarisha usafi wa Mazingira kwa kila kaya.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa katika kijiji cha Mbuyuni kilichopo katika Kata hiyo ya Mbuyuni
kaya nyingi hazina vyoo hivyo kupelekea choo kimoja kinachangiwa na kaya zaidi ya mbili hadi tatu.
"Kila ifikapo tarehe 26 Septemba kila mwaka huwa tunafanya maadhimisho ya siku ya Afya Mazingira duniani, hiki tunachokifanya hapa kwenu na hata maeneo mengine tunafanya, lakini kwa kata yote ya Mbuyuni na hasa kijiji hiki cha mbuyuni takwimu zake za usafi sio nzuri sana hivyo bado mnakazi ya kufanya ili kuendelea kutunza afya zetu'."
"Lazima tufahamu Mazingira yana uhusiano moja kwa moja na afya ya binadamu, Mazingira yasipokuwa safi basi afya ya binadamu itatetereka
kwaiyo haya tunayoyasisitiza wala hayana gharama" alisisitiza
Aidha, ameendelea kuwakumbusha Wananchi kuachana na ujenzi wa vyoo vya nyasi ambavyo si bora na salama ambavyo kupelekea mvua zinaponyesha vyoo hivyo kuanguka na kubaki wazi sehemu ya juu na hivyo kupoteza ubora wa vyoo hivyo.
Hata hivyo pamoja na kuwataka wajenge vyoo kwa kutumia vifaa vya Kudumu Bw. Ame alihitimisha kwa kuwaelezea sifa za choo bora zikiwemo shimo refu, kiwe na mlango, kiwe na sakafu ili kiwe rahisi kusafishwa pamoja kuezekwa ili kipindi cha mvua choo kiweze kutumika.
28/09/2025
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa